Umoja wa Mataifa waonyesha wasiwasi wake kutokana na kuendelea machafuko Sudan Kusini
Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameonyesha wasiwasi mkubwa alionao kutokana na kuendelea mgogoro wa Sudan Kusini na ametoa wito wa kusimamishwa mapigano katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Zeid Raad al-Hussein ametoa taarifa inayozitaka pande zote zinazozozana huko Sudan Kusini kusimamisha mapigano na kuchukua hatua za lazima za kuutatua mgogoro wa nchi hiyo kwa njia za kisiasa na hivyo kuokoa maisha ya raia wa nchi hiyo.
Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, kuna haja ya kuchukuliwa hatua za kusimamishwa mapigano haraka huko Sudan Kusini.
Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umetangaza katika ripoti yake kwamba, takribani nusu ya raia wa Sudan Kusini wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na kwamba, baa la njaa ndio tishio kubwa kwa raia hao.
Mapigano yalianza nchini Sudan Kusini mwaka 2013 kati ya jeshi linalomuunga mkono Rais Salva Kiir na wanamgambo watiifu kwa aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar.
Japokuwa mahasimu hao wakuu wa kisiasa walisaini hati ya makubaliano mwaka 2015 lakini amani na utulivu haujarejea tena nchini humo.
Maelfu ya watu waliuawa na mamia ya maelfu ya wengine waliuhama mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba na kukimbilia maeneo mengine baada ya kuzuka mapigano kuanzia tarehe 8 hadi 11 za mwezi Julai mwaka jana baina ya askari watiifu kwa Rais Salva Kiir na wapiganaji wanaomuunga mkono Riek Machar..