Kuendelea mashauriano ya kurudisha uthabiti Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28696-kuendelea_mashauriano_ya_kurudisha_uthabiti_libya
Katika kuendelea juhudi za kuleta amani na uthabiti huko Libya, Mwakilishi Malum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Libya ameonana na kufanya mazungumzo na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 05, 2017 23:32 UTC
  • Kuendelea mashauriano ya kurudisha uthabiti Libya

Katika kuendelea juhudi za kuleta amani na uthabiti huko Libya, Mwakilishi Malum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Libya ameonana na kufanya mazungumzo na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya nchi hiyo.

Martin Kobler, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Libya amekutana na Fayez Mustafa as-Sarraj Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya katika mji mkuu wa nchi hiyo na kujadiliana naye kuhusiana na matukio mapya ya kisasa na kiusalama nchini humo. Baada ya mazungumzo hayo, Kobler amesisitiza kuwa ofisi yake nchini Libya inafanya juhudi za kuyakutanisha pamoja makundi yote hasimu ya nchi hiyo ili kubuni na kuwasilisha mpango ambao utatekelezwa na makundi hayo. Kwa pande wake as-Sarraj amesema kuwa wakati umewadia kwa pande zote hasimu za nchi hiyo kushirikiana kwa ajili ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo.

Mertin Kobler, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN Libya

Matamshi hayo yanatolewa katika hali ambayo Khalifa Haftar kamanda wa jeshi la Libya pia hivi karibuni alikutana na kufanya mazungumzo na as-Sarraj na kusisitiza udharura wa kuwekwa kando tofauti zao kwa ajili ya kutatua matatizo ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa mazungumzo hayo viongozi wawili hao wa Libya wataunda jeshi moja la kitaifa na kisha kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi mkuu wa bunge na rais baada ya kupita miezi sita tokea wakati wa kufanyika mazungumzo hayo. Kuundwa Baraza la Urais litakalojumuisha kamanda wa jeshi, waziri mkuu na spika wa bunge na vilevile kupambana na ugaidi na kuvunjwa makundi yote yanayobeba silaha ni masuala mengine yaliyofikiwa katika mazugumzo hayo. Hata kama mgogoro wa Libya ulianza mwaka 2011 mara tu baada ya kupinduliwa na kuuawa Muammar Qaddafi dikteta wa zamani wa nchi hiyo kupitia uingiliaji wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi lakini ni wazi kuwa nchi hiyo inakaribia kugawanyika vipande vipende kutokana na kuendelea mgogoro huo.

Fayez as-Sarraj akiwa na Khalifa Haftar

 

Kabla ya hapo juhudi za kieneo na kimataifa pia zilikuwa zimefanyika kwa ajili ya kuleta uthabiti na amani nchini Libya jambo lililopelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hata hivyo serikali hiyo haijapewa fursa ya kujiimarisha na kuendesha vizuri shughuli zake katika pembe tofauti za nchi hiyo kutokana na kuwepo makundi ya wanamgambo, magaidi, mirengo ya kikabila inayozozana kwa ajili ya kupewa hisa katika utawala wa nchi hiyo na vilevile uingiliaji wa nchi za Magharibi na kieneo. Hivi sasa kuwepo kwa mazingira mapya ya kisiasa katika eneo na kuenea makundi ya kigaidi katika eneo na pembe tofauti za dunia kunaendelea kuvuruga juhudi za kuleta amani na utulivu wa kudumu huko Libya. Hali isiyo ya kuridhisha ya usalama katika baadhi ya nchi za eneo imeimarisha shughuli za baadhi ya makundi ya kigaidi likiwemo la Daesh kwa kadiri kwamba ni hivi karibuni tu ambapo visima vingi vya mafuta ya Libya vilikuwa mikononi mwa kundi hilo hatari la kigaidi, hata hivyo vilidhibitiwa baadaye na jeshi la nchi hiyo.

Magaidi wa Daesh wakieneza udhibiti wao Libya

Pamoja na hali hiyo kuna wasiwasi huu kuwa huenda visima hivyo vikadhibitiwa tena na makundi hayo ya kigaidi iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa kwa ajili ya kulinda usalama katika maeneo hayo ya mafuta. Suala hilo limezipelekea baadhi ya nchi za Magharibi na vibaraka wao wa eneo kuhisi hatari hiyo na hivyo kuzifanya zilegeza misimamo yao katika kudai hisa katika utajiri wa Libya. Hata kama kungali kuna njia ndefu kabla ya utatuzi wa mgogoro wa Libya kufikiwa lakini mapatano yaliyofikiwa siku chache zilizopita na kutolewa wito wa kutatuliwa kwa njia za amani mgogoro huo, yote hayo yanaweza kuwa ni hatua ya kwanza muhimu katika njia ya utatuzi wa mgogoro huo katika mazingira ya sasa.