Makumi ya askari wa Libya wauawa na kujeruhiwa Benghazi
Kwa akali askari 11 wa jeshi la Libya wameuawa na wengine 55 kujeruhiwa katika makabiliano na magenge ya kigaidi mjini Benghazi, mashariki mwa nchi.
Kanali Miloud Zouai, Msemaji wa Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ugaidi nchini humo amesema askari watiifu kwa Jenerali Mstaafu Khalifa Haftar, Mkuu wa Jeshi la Libya mashariki mwa nchi hiyo, hapo jana walianzisha hujuma dhidi ya ngome mbili kuu za mwisho za magenge ya kigaidi katika eneo la Al-Sabri, viungani mwa mji wa pwani wa Benghazi, ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Libya.
Vikosi tiifu kwa Khalifa Haftar ambavyo havitambui Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa vimekomboa sehemu kubwa ya mji huo tangu uingie mikononi mwa magenge ya kigaidi na kitakfiri yakiongozwa na Daesh (ISIS) mwaka 2014.
Mashambulizi hayo dhidi ya askari wa Libya yanajiri katika hali ambayo, Khalifa Haftar na Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya walikutana Jumanne iliyopita mjini Abu Dhabi Imarati na kufikia makubaliano kuhusu utatuzi wa hitilafu za pande hizo mbili, kukiwemo kuunda jeshi moja na kusimamia kwa pamoja uchaguzi wa Rais na Bunge katika kipindi cha miezi sita ijayo.
Itakumbukwa kuwa, mji wa kistratajia wa Benghazi ulitumiwa kuanzisha vuguvugu na kampeni za kumpindua Kanali Muammar Gaddafi, kiongozi wa zamani wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika mwaka 2011.