Iran na Ethiopia zasisitiza juu ya kuimarisha ushirikiano wao
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ethiopia zimesisitiza juu ya kuimarisha ushirikiano baina yao katika nyanja mbalimbali.
Hayo yamefikiwa katika mazungumzo kati ya balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Ethiopia na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo ya Kiafrika.
Balozi Behzad Khakpour na Workneh Gebeyehu wamesisitiza katika mazungumzo yao katika mji mkuu Addis Ababa juu ya azma ya nchi zao ya kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili katika nyuga mbalimbali.
Balozi Khakpoiu ambaye pia ni mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya katika Umoja wa Afrika amesema katika mazungumzo hayo kwamba, daima uhusiano wa Iran na Ethiopia umeshuhudia urafiki na mahusiano ya karibu na ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana kumekuweko na mazingira na anga nzuri ya kufanyika juhudi za kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili katika nyanja tofauti.
Kwa upande wake Workneh Gebeyehu, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ethiopia amesema katika mazungumzo yake na balozi wa Iran mjini Addis Ababa kwamba, kuimarishwa ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ukiwemo uga wa kiuchumi ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele na serikali ya nchi hiyo.
Aidha Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ethiopia anatazamiwa kuitembelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika wasaa na fursa ya kwanza atakayopata.