UNESCO yaafiki ombi la Rwanda kuhusu kumbukizi za mauaji ya kimbari 1994
Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ametangaza kuunga mkono ombi la Rwanda la kutaka maeneo manne yenye kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 yajumuishwe katika orodha ya Turathi za Dunia ya shirika hilo.
Irina Bokova, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO amesema kuna haja maeneo hayo yajumuishwe katika madaftari ya kumbukumbu ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa, ili kutoa tahadhari kwa nchi nyingine zisijikute zinatumbukia katika mauaji ya kimbari kama yaliyoshuhudiwa nchini Rwanda mwaka 1994.
Baada ya kutembelea Jumba la Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari mjini Kigali hapo jana, Irina Bokova alisema atawasilisha mapendekezo yake kwa Kamati ya Turathi za Dunia ya UNESCO ili kuona maeneo hayo ya kumbukizi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda yanajumuishwa katika orodha hiyo kwa lengo la kukifungua macho kizazi cha sasa na kuvitahadharisha vizazi vijavyo.
Serikali ya Rwanda inatumai itakuwa imetimiza masharti yote ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni kufikia mwaka ujao 2018, ili maeneo hayo manne ya kumbukizi hizo yajumuishwe katika orodha ya UNESCO.
Maeneo hayo ni Kigali Genocide Memorial Centre eneo la Gisozi, Ntarama Genocide Memorial iliyoko katika wilaya Bugesera, Murambi Genocide Memorial iliyoko wilayani Nyamagabe na Bisesero Genocide Memorial katika wilaya Karongi.
Itakumbukwa kuwa, karibu watu milioni moja, wengi wao wakiwa ni wa kabila la Tutsi pamoja na Wahutu wenye misimamo ya wastani waliuawa katika mauaji ya kimbari ya siku 100 mwaka 1994 nchini Rwanda.