May 12, 2017 03:42 UTC
  • Rais wa Somalia aomba msaada wa kimataifa

Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia ameiuomba jamii ya kimataifa iisaidie nchi yake katika kupambana na ugaidi, ufisadi na umaskini wa kuchupa mipaka; mambo ambayo amesema ndiye adui mkuu wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa IRIB, Mohamed Abdullahi Mohamed alisema hayo jana katika mkutano wa kimataifa kuhusu Somalia uliofanyika mjini London Uingereza kwa shabaha ya kurejesha amani na utulivu nchini humo.

Amesema, nchi yake inahitajia msaada wa kimataifa katika jitihada zake za kuwaletea ustawi wananchi wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Ikumbukwe kuwa Somalia ni moja ya nchi maskini zaidi na moja ya nchi zenye ukosefu mkubwa zaidi wa amani duniani.

Wananchi wa Somalia wanazumbuliwa na majanga ya kila namna

 

Hali nchini humo ni mbaya sana kiasi kwamba Umoja wa Mataifa umesema katika mkutano huo wa mjini London Uingereza kuwa, unahitajia dola milioni 900 za Kimarekani kufikia mwishoni mwa mwaka huu kwa ajili ya kunusuru maisha ya raia milioni 6 wa Somalia wanaohitajia misaada ya dharura ya kibinadamu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema, Wasomali milioni 6 wanahitajia misaada ya haraka sana ya kibinadamu wakiwemo watoto wadogo zaidi ya laki 2 na 75 elfu, wanaosumbuliwa na utapiamlo na lishe duni.

Amesema watoto wa Kisomali wanakodolewa macho na janga la uhaba wa chakula, maji sambamba na magonjwa mbalimbali yaliyosababishwa na mazingira machafu.

Kongamano hilo limewaleta pamoja wadau wa kimataifa, Umoja wa Mataifa na nchi wafadhili ili kujaribu kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na kuiwezesha kufikia malengo yake ya maendeleo, usalama na kustawisha uchumi ifikapo mwaka 2020.

Tags