Wapinzani waungana dhidi ya serikali nchini Sudan Kusini
Makundi saba ya upinzani nchini Sudan Kusini yamezika tofauti zao na kusema kuwa yatashirikiana kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali ya sasa ya Rais Salva Kiir.
Makundi hayo ya kisiasa ni pamoja na chama cha kiongozi wa waasi nchini humo Riek Machar ambaye alikimbia nchi akidai kuwa vyombo vya usalama vilikuwa vinakula njama ya kumuua.
Shakhsia wengine waliotangaza kuuunga mkono muungano huo wa upinzani ni mawaziri wa zamani wa nchi hiyo Kosti Manibe na Lam Akol, pamoja na Thomas Cirillo Swaka, aliyekuwa kamanda wa ngazi za juu wa jeshi la nchi hiyo. Swaka ambaye alijiuzulu mwezi Februari mwaka huu, kutokana na kile alichokitaja kuwa ukiukaji wa haki za binadamu ndani ya jeshi hilo, alikuwa Kamanda Mkuu wa Lojistiki.
Nathaniel Oyet, afisa wa ngazi za juu ndani ya chama cha SPLA-IO chake Riek Machar amesema makundi ya wapinzani yamekubaliana kuungana pamoja kisiasa, kidiplomasia na kijeshi ili umoja wao utoe pigo kwa serikali.
Hata hivyo Msemaji wa Rais, Ateny Wek Ateny ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, serikali haiko tayari kufanya mazungumzo na kundi lolote jipya la upinzani wala kulitambua.
Sudan Kusini ilitumbukia katika machafuko mwezi Disemba mwaka 2013, baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu aliyekuwa makamu wake Riek Machar kwamba alikula njama za kutaka kumpindua. Katika machafuko hayo, maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.