Umoja wa Mataifa kuwasaidia wakazi wa eneo la Ziwa Chad
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, kumetengwa bajeti maalumu ya kuwasaidia wakazi wa eneo la Ziwa Chad ambao kwa sasa wanakabiliwa na hali mbaya kimaisha.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kibinadamu na mratibu wa misaada ya kibinadamu amesema kuwa, umoja huo umetenga bajeti ya dola milioni kadhaa kwa ajili ya kuwasaidia wakazi wa Ukanda wa Ziwa Chad.
Stephen O'Brien ameongeza kuwa, bajeti ya dola milioni 3.5 imeandaliwa kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kwa wakazi elfu 40 wa Ukanda wa Ziwa Chad wanaotatizika kudhamini mahitaji yao ya lazima ya kila siku.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa watu milioni 11 katika eneo la Ziwa Chad linalojumuisha Cameroon, magharibi mwa Chad, kusini mashariki mwa Niger na kaskazini mashariki mwa Nigeria wanahitajia misaada ya haraka ya chakula.
Hivi karibuni, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetahadharisha kuwa kukosekana usalama wa chakula katika eneo la Ziwa Chad kunasababishwa na mashambulizi na hujuma za kundi la kigaidi la Boko Haram.
Kwa mara nyingine tena Umoja wa Mataifa umezitaka nchi wanachama wa umoja huo kushiriki katika harambee ya kudhamini misaada ya kifedha itakayotumika kuwasaidia wananchi wa eneo hilo ambao wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu kutokana na kukosa huduma muhimu.