Algeria: Nguvu za kijeshi Syria, Yemen na Libya zmesababisha maafa
Spika wa Bunge la Algeria ametangaza kuwa, kutumiwa nguvu za kijeshi katika nchi za Syria, Yemen na Libya kumesababisha kutokea maafa ya kibinadamu katika nchi hizo.
Abdul Qadir bin Saleh amesema bayana kwamba, machaguo ya nguvu za kijeshi kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi migogoro ya Syria, Libya na Yemen katu hayajawa na matokeo mazuri.
Amesema, si tu kwamba, hatua hizo hazijasaidia kuipatia ufumbuzi migogoro hiyo bali zimesababisha nchi hizo kukumbwa na maafa ya kibinadamu kutokana na raia wasio na hatia kuendelea kuuawa kila siku.
Spika wa Bunge la Algeria aisha amesisitiza kwamba, njia pekee ya kuipatia ufumbuzi migogoro ya nchi hizo ni mazungumzo kwani hatua za kijeshi kama ilivyothibitika kwa mara nyingine tena hazina matokeo ghairi ya maafa na uharibifu mkubwa.
Abdul Qadir bin Saleh amezungumzia mashambulio ya kijeshi ya Saudia na waitifaki wake dhidi ya Yemen, kusimamishwa uanachama wa Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu pamoja na hujuma ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Syria na kueleza kuwa, nchi yake inapinga vikali yote hayo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, ripoti mbalimbali za Umoja wa Mataifa zinaeleza juu ya kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu katika nchi za Syria, Libya, na Yemen.
Baadhi ya ripoti hizo zinaashiria juu ya kutokea maafa ya kibinadamu katika nchi hizo.