UN yatahadharisha kuhusu kusimamishwa misaada ya kibinadamu nchini Nigeria
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, kupunguzwa bajeti za umoja huo kumezikwamisha taasisi zake katika kuendesha miradi mbalimbali ya kimataifa ikiwa ni pamoja na kuwatumia chakula waathirika wa mashambulizi ya kundi la Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa imesema mjini Lagos Nigeria kuwa, mamilioni ya wananchi wa mikoa mitatu ya Yobe, Borno na Adamawa ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo wanahitajia misaada ya haraka ya chakula, lakini kutokana na kukosekana fedha za kutosha, mashirika ya misaada ya kibinadamu yamelazimika kufunga ofisi zao kwenye mikoa hiyo.
Ripoti ya ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, kukosekana fedha kumeathiri vibaya juhudi zote zilizofanyika hadi hivi sasa na hivi sasa ripoti zinaonesha kuzidi kuwa mbaya hali ya wakazi wa mikoa hiyo ambao wanashindwa kuendesha kazi zao za kawaida kama vile kilimo kutokana na sababu mbalimbali yakiwemo mashambulizi ya mara kwa mara ya magaidi wa Boko Haram.
Kundi hilo la kigaidi lilianzisha mashambulizi yake mwaka 2009 nchini Nigeria. Watu wasiopungua 20 elfu wameshauwa nchini Nigeria tangu wakati huo hadi hivi sasa na zaidi ya milioni mbili na laki sita wengine wamelazimika kuyakimbia makazi yao. Mwaka 2015 genge hilo la Boko Haram lilipanua mashambulizi yake hadi katika nchi jirani za Chad, Niger na Cameroon.