Nchi jirani zaunga mkono mazungumzo ya amani Libya
Nchi zinazopakana na Libya zimeunga mkono juhudi za kumaliza migogoro ya nchi hiyo kupitia kuanzisha mazungumzo ya pande zote ya kisiasa.
Nchi jirani na Libya ambazo zimeshiriki kwenye kikao cha viongozi wa kundi la G7 mjini Taormina katika kisiwa cha Sicily nchini Italia, jana walizitaka nchi wanachama wa kundi hilo hususan Ufaransa na Uingereza kusaidia juhudi za kukomesha mgogoro wa Libya ambao unaziathiri vibaya nchi jirani.
Rais Mahamadou Issoufou wa Niger ambaye nchi yake ni jirani wa kusini mwa Libya amesema katika kikao hicho kwamba vita dhidi ya ugaidi kaskazini mwa Afrika vinahitajia kuchukuliwa hatua za haraka za kukomesha migogoro nchini Libya na kuingia madarakani serikali yenye nguvu itakayokuwa na uwezo wa kudhibiti maeneo yote ya nchi hiyo.
Rais wa Niger amewataka wanachama wa kundi la G7 na Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za lazima ikiwa ni pamoja na kuzisaidia nchi kama za Niger, Mali, Mauritania na Chad kukabiliana na magenge ya kigaidi yanayotumia ardhi ya Libya kama maficho yao.
Kwa upande wake, Umoja wa Ulaya umeyataka makundi hasimu nchini Libya kuacha mapigano, kuheshimu usitishaji vita na kujali maslahi ya taifa. Vile vile umewataka viongozi wa kisiasa nchini Libya kufuata mkondo wa Umoja wa Mataifa wa kumaliza migogoro ya nchi yao kwa njia ya mazungumzo.