Kuendelea ukandamizaji wa malalamiko ya wapinzani nchini Ethiopia
Ukandamizaji wa malalamiko ya wapinzani umeshuhudiwa tena katika eneo la Oromia, Ethiopia baada ya kutangazwa hali ya hatari na serikali na hivyo kuzusha wasi wasi na wahka kwa wakazi wa eneo hilo.
Migogoro ya kisiasa imekuwepo kwa muda mrefu sasa katika miji tofauti nchini Ethiopia. Licha ya serikali Addis Ababa kutangaza hali ya hatari na kufanya ukandamizaji wa kisiasa uliokithiri, bado serikali ya nchi hiyo imeshindwa kudhibiti hali ya mambo nchini humo. Malalamiko ya wananchi na pia matatizo ya kiuchumi na kijamii kwa muda sasa yameyaweka maisha ya wananchi wa nchi hiyo katika mashinikizo, hata hivyo hatua ya serikali ya kutwaa ardhi za wakulima wa kabila la Oromia kwa kisingizio cha upanuzi wa mji, ndiyo iliyowasha moto wa malalamiko ya Waethiopia. Tofauti za kikaumu na kikabila zinatajwa kuwa sababu kuu ya malalamiko nchini Ethiopia.
Hii ni kusema kuwa, kwa muda sasa watu wa kaumu za Oromo na Amhara wamekuwa wakilalamikia sana ubaguzi wa kikabila nchini humo. Jamii ya wachache ya Amhara ni kundi la pili kubwa nchini Ethiopia baada ya watu wa kaumu ya Oromo ambapo kila moja linalalamikia sana ubaguzi wa serikali kwa maslahi ya watu wa kabila la Tigrinya. Kwa mujibu wa makabila hayo, watu wa kabila la Tigrinya wanapendelewa na serikali kwa kupewa nafasi katika maeneo muhimu ya serikali kama vile jeshini. Maandamano ya wananchi huko Ethiopia yanashuhudiwa sana katika mikoa ya Amhara na Oromia ambayo wakazi wake wanaunda asilimia 60 ya wananchi wa nchi hiyo, suala ambalo limesababisha ukosefu wa utulivu na usalama wa kisiasa nchini humo.
Wapinzani pia wanalalamikia muamala mbaya wa serikali katika sekta za kiuchumi na kijamii, ambapo wanaamini kuwa licha ya nchi hiyo kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili, lakini bado uchumi wake ni mbaya sana, huku hadi sasa maeneo mengi yakiwa yangali yanakabiliwa na ukame na wakazi wake kukumbwa na njaa. Mbali na hayo ni kwamba wapinzani nchini Ethiopia wanalalamikia uhuru wa kisiasa na kijamii wanaonyimwa na serikali ya nchi hiyo. Ili kudhibiti hali ya mambo, serikali ya Addis Ababa ilitangaza hali ya hatari kuanzia mwezi Oktoba mwaka jana ambayo ilidumu kwa miezi sita. Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Hailemariam Desalegn ndiye aliyetangaza amri hiyo. Baada ya kumalizika muda huo wa miezi sita, hali hiyo ya hatari iliongezwa muda na bunge la nchi hiyo. Lengo la hali hiyo ya hatari ni kuondoa kabisa mikusanyiko dhidi ya serikali na kuimarisha usalama na amani nchini humo.
Licha ya kuchukuliwa hatua hizo lakini serikali bado iliendeleza ukandamizaji dhidi ya wapinzani na kuwatia mbaroni. Kwa mujibu wa takwimu rasmi za hivi karibuni kabisa zilizotolewa na kamisheni ya haki za binaadamu nchini humo, maandamano ya wananchi ya mwaka jana yalikuwa ya umwagaji damu mkubwa ambapo kwa akali watu 669 waliuawa, huku 462 kati yao wakiwa ni wakazi wa eneo la Oromia pekee. Kadhalika zaidi ya watu elfu 26 miongoni mwa waandamanaji walitiwa mbaroni na polisi wa serikali. Waandamanaji nchini Ethiopia wanataka pia kukomeshwa ubaguzi wa kikaumu na kikabila na kadhalika kufanyika marekebisho ya kisiasa na kijamii ikiwemo kuhitimishwa ukiukaji wa haki za binaadamu, mauaji ya raia, kamatakamata ya kiholela na ukandamizaji wa kisiasa dhidi ya makundi ya upinzani ya serikali. Licha ya kupita miezi kadhaa tangu yalipoongezeka malalamiko ya wananchi na ukandamizaji wa polisi, serikali ya Addis Ababa bado haijayafanyia kazi malalamiko ya wananchi na kinyume chake imeendeleza ukandamizaji na kuandaa mazingira ya hofu na kuwatisha wapinzani.
Katika hali ambayo raia wa Ethiopia wamekasirishwa na hatua za serikali, mazingira ya usalama, na ukandamizaji dhidi ya wapinzan licha ya kupigania matakwa yao kwa njia za usalama na kuheshimu sheria, lakini serikali ya Addis Ababa haioneshi nia ya kuwasikiliza wapinzani. Inaonekana wazi kwamba, wanachopaswa kufanya viongozi wa Ethiopia ni kuacha kutumia mabavu na badala yake wazingatie matakwa ya wananchi sambamba na kufanyia marekebisho siasa kupitia kupunguza ubaguzi wa kikaumu na kikabila na kuandaa mazingira ya usawa kwa ajili ya raia wote wa nchi hiyo.