UN yaonya kuhusu kuendelea mapigano Jamhuri ya Afrika ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29738-un_yaonya_kuhusu_kuendelea_mapigano_jamhuri_ya_afrika_ya_kati
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu kuanza upya mapigano ya kikabila na kidini katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
May 29, 2017 02:48 UTC
  • UN yaonya kuhusu kuendelea mapigano Jamhuri ya Afrika ya Kati

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu kuanza upya mapigano ya kikabila na kidini katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Najat Rochdi Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu Katika Umoja wa Mataifa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) katika taarifa amebainisha wasiwasi wake kutokana na kuanza upya machafuko na ukiukwaji haki za binadamu katika nchi hiyo.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ametaka machafuko hayo yasitishwe mara moja na mazungumzo ya amani yaanze. Amelaani hasa machafuko katika maeneo ya Alindao, Bangassou, Mobaye na Bri na kuongeza kuwa hujuma yoyote dhidi ya watu kwa msingi wa kabila au dini ni ukiukwaji wa haki za binadamu.  

Waziri wa Masuala ya Kijamii na Maelewano ya Kitaifa Jamhuri ya Afrika ya Kati Virginia Mbaikoua anasema kufuatia machafuko ya wiki za hivi karibuni nchini humo, malaki ya watu wamekimbia makazi yao, huku watu 300 wakiuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Askari wa UN wanaolinda amani CAR wameshindwa kuzuia machafuko

Kwa mujibu wa ofisi ya UN huko CAR, katika hujuma dhidi ya eneo lenye Waislamu wengi la Bangassou, watu 108 waliuawa na wengine 76 kujeruhiwa. 

Machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yaliibuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoka madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo, François Bozizé, huku mgogoro ukishadidi baada ya waasi wa Kikristo wenye kufurutu ada wa Anti-Balaka kuanzisha mauaji ya kutisha dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya watu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi.