Kundi la wabeba silaha Libya lamwachia huru Saiful Islam Gaddafi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30318-kundi_la_wabeba_silaha_libya_lamwachia_huru_saiful_islam_gaddafi
Kundi moja la wabeba silaha nchini Libya limetangaza kuwa limemwachia huru mwana wa kiume wa aliyekuwa dikteta wa nchi hiyo aliyeuawa Muammar Gaddafi, Saiful-Islam Gaddafi ambaye alikuwa akishikiliwa gerezani tangu mwaka 2011.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 11, 2017 03:33 UTC
  • Kundi la wabeba silaha Libya lamwachia huru Saiful Islam Gaddafi

Kundi moja la wabeba silaha nchini Libya limetangaza kuwa limemwachia huru mwana wa kiume wa aliyekuwa dikteta wa nchi hiyo aliyeuawa Muammar Gaddafi, Saiful-Islam Gaddafi ambaye alikuwa akishikiliwa gerezani tangu mwaka 2011.

Al-Ajmal Al-Atiri, kamanda wa kundi la wanamgambo wanaobeba silaha linalojiita "Abubakr Al-Siddiq" linaloundwa na makundi kadhaa ya waasi na ambalo lilikuwa likimshikilia mwana huyo wa kiume wa Gaddafi tangu miaka sita nyuma wakati akijaribu kukimbia kupitia majangwani amethibitisha kuwa Saiful-Islam Gaddafi aliachiwa huru siku ya Ijumaa usiku kwa mujibu wa sheria ya msamaha kwa wafungwa wa kisiasa uliotolewa na Bunge la mashariki mwa nchi hiyo.

Ripoti zinaeleza kuwa Ijumaa hiyohiyo Saiful-Islam Gaddafi aliondoka katika mji wa Zintan ulioko kaskazini magharibi mwa Libya na kuelekea kusikojulikana.

Muammar Gaddafi

Kwa mujibu wa kundi hilo la wanamgambo linalodhibiti mji wa Zintan, Saiful-Islam ameachiwa huru kuitikia ombi la Wizara ya Sheria ya serikali ya mpito ya Libya yenye mfungamano na bunge la nchi hiyo na kufuatia kupitishwa sheria ya msamaha kwa wafungwa wa kisiasa. 

Ripoti za kuachiwa huru na kuondoka Zintan Saiful-Islam Gaddafi ambazo bado hazijathibitishwa na duru huru zinaonekana hazikuwafurahisha baadhi ya watu wa mji wa mji huo lakini taarifa zinaeleza kuwa hatua hiyo imepokewa kwa furaha katika mji wa kusini magharibi wa Sebha ambako watu walikuwa wakifyatua risasi hewani katika mitaa ya mji huo kusherehekea kuachiwa huru mwana huyo wa kiongozi wa zamani wa Libya aliyeondolewa madarakani na kuuawa mwaka 2011.../