Ethiopia kuishiwa na misaada ya dharura ya chakula
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30856-ethiopia_kuishiwa_na_misaada_ya_dharura_ya_chakula
Mashirika ya Kimataifa yametahadharisha kuwa, Ethiopia itaishiwa na misaada ya chakula ya dharura katika kipindi cha mwezi ujao, hali ambayo itawasibu karibu watu milioni nane walioathiriwa na ukame.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2017 03:37 UTC
  • Ethiopia kuishiwa na misaada ya dharura ya chakula

Mashirika ya Kimataifa yametahadharisha kuwa, Ethiopia itaishiwa na misaada ya chakula ya dharura katika kipindi cha mwezi ujao, hali ambayo itawasibu karibu watu milioni nane walioathiriwa na ukame.

Mashirika hayo yalisema jana kuwa ukame umesababisha watu milioni 7.8 nchini Ethiopia kutegemea misaada ya chakula ili kuishi. John Graham Mkurugenzi wa Shirika la Save the Children nchini humo amesema kuwa chakula kinatazamiwa kuisha katika muda wa mwezi mmoja na kwamba hawajui nini kitatokea baadaye. Raia wa Somalia wanaoishi maeneo ya kusini mashariki mwa Ethiopia wameeleza kuwa, hali ya ukame haijamuacha yoyote salama. Ukame huo unaoendelea umeuwa mifugo mingi, kukausha mabwawa na kuwalazimisha maelfu ya raia kuishi makambini.

Raia wakikabiliwa na hali ngumu ya ukame makambini nchini Ethiopia 

Hali ya ukame imekuwa jambo la kawaida huko Ethiopia ambapo mwaka 1984 hadi 1985 janga hilo liliuwa mamia ya maelfu ya watu  nchini humo. Mwaka 2015 hadi 16 serikali ya Ethiopia ilitumia kiasi kikubwa cha pesa yaani dola milioni 766 kukabiliana na moja ya majanga mabaya zaidi ya ukame kuwahi kuiathiri nchi hiyo katika miongo kadhaa iliyopita.