Baraza la Usalama la UN larefusha vikwazo dhidi ya Libya
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limerefusha vikwazo dhidi ya Libya.
Kikao cha dharura cha jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilipiga kura na kuridhia kuirefushia vikwazo Libya hadi Novemba 15 mwaka 2018, hatua iliyokosolewa na Mwakilishi wa Libya katika Umoja wa Mataifa. Marufuku ya kusafirisha mafuta ghafi na bidhaa zitokanazo na mafuta pia imejumuisha kwenye marufuku hiyo.
Lengo la hatua hiyo ya Baraza la Usalama ni kuzuia biashara haramu ya bidhaa zinazotokana na mafuta ya Libya ili kukata vyanzo vya kifedha kwa makundi yenye silaha nchini humo. Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaruhusu kutumiwa nguvu za kijeshi ili kuruhusu kutekelezwa vipengee vya azimio hilo na wakati huo huo linasisitiza kuwa, hali ya mambo nchini Libya bado ni tishio kwa amani na usalama wa kimataifa.
Baraza la Usalama katika azimio lake nambari 2362 limeitaka serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya inayoongozwa na Fayez al Siraj iimarishe suala la kusimamia taasisi za kifedha za nchi hiyo hususan Shirika la Mafuta la Taifa, Benki Kuu na Taasisi ya Vitega Uchumi ya nchi hiyo.