Jul 01, 2017 03:37 UTC
  • Afrika Kusini kuomba msaada wa nje kuunusuru uchumi

Afrika Kusini imetangaza kuwa huenda ikahitajia misaada ya kifedha kutoka nje ya nchi ili kuunusuru uchumi wa nchi hiyo unaoyumbayumba.

Waziri wa Uchumi Malusi Gigaba alisema Ijumaa kuwa, kunahitajika hatua za haraka kuupiga jeki uchumi ili uanze tena kustawi.

Wakati huo huo Rais Jacob Zuma anayepigana kujinusuru kisiasa amekiri kuwa uchumi wa nchi hiyo hautafikia kiwango kilichowekwa na serikali cha kustawi kwa asilimia 1.3. Ametoa wito kwa waitifaki wake wa kisiasia kujadili njia za kufufua uchumi ikiwa ni pamoja na kugawa upya ardhi ya nchi hiyo. Ametaka kuchukuliwe maamuzi ya kimsingi lakini kwa mujibu wa katiba ili kuhakikisha Waafrika wazalendo waliowengi nchini humo wanapata ardhi.

Naibu Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa

Zuma na waziri wake wa fedha walikuwa wakizungumza katika kongamano la chama tawala cha ANC ambalo linalenga kumtafuta mtu atakayechukua nafasi ya Zuma kama mwenyekiti wa chama mwezi Disemba. Naibu wa Rais wa Afrika Kusini Cyrila Ramaphosa na mkuu wa zamani wa tume ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma, ambaye aliwahi kuwa mke wa rais Zuma, wanatajwa kuwa wanaongoza katika kuwania nafasi hiyo. Atakayechaguliwa kama mwenyekiti wa ANC atakuwa na nafasi kubwa ya  kuwa rais wa nchi hiyo baada ya kipindi cha Zuma kumalizika mapema mwaka 2018.  Uchumi wa Afrika Kusini umedorora na kiwango cha ukosefu wa ajira ni asilimia 28 huku nchi hiyo ikikumbwa na mivutano ya kisiasa.

 

Tags