Waziri wa Afya: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haina tena Ebola
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza rasmi kumalizika kwa maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ebola nchini humo.
Oly Ilunga Kalenga, Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ametoa hakikisho hilo baada ya kusema kuwa, hakuna kesi yoyote ya maambukizi mapya yaliyoshuhudiwa ndani ya siku 42.
Ugonjwa wa Ebola uliripotiwa kuibvuka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwezi Mei katika eneo la Kaskazini Mashariki, na kusababisha vifo vya watu wanne na zaidi ya 20 kuambukizwa.
Shirika la Afya duniani WHO limeipongeza serikali ya Kinshasa kwa namna ilivyoshughulikia maambukizi haya na kutoa taarira za mara kwa mara kwa raia wake.
Ebola iliripotiwa kwa mara ya kwanza nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwaka 1976 na kusambaa katika maeneo mengine ya dunia.
Mnamo mwaka 2014, mlipuko wa ugonjwa huo huko Kongo DR ulidhibitiwa kwa haraka ingawa watu 49 walifariki dunia.
Itakumbukwa kuwa, watu zaidi ya 11,000 walifariki dunia kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika eneo la Afrika Magharibi mwaka 2014 hadi 2015, hususan nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia katika mlipuko wa Ebola ulioatajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani.