Huenda mlipuko wa Ebola nchini DRC ukadumu kwa mwaka mmoja
-
Kongo na changamoto ya ugonjwa wa Ebola
Imebainika kuwa mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola unaoendelea kuenea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) bado haujafikia kilele chake, na huenda ukadumu kwa takriban mwaka mmoja.
Hayo yamedokezwa na Bruno Michon, Meneja wa Operesheni za Mlipuko wa Ebola katika Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC). Akizungumza na waandishi wa habari Jumanne kupitia mawasiliano ya video kutoka mashariki mwa DRC amesema kwamba:
“Ni vigumu kufahamu kwa usahihi kiwango ambacho mlipuko unaenea… lakini naamini kuwa kilele chake hakijapita; bado kiko mbele yetu.”
Ameongeza kuwa: “Tunahofia kuwa huenda ikachukua hadi mwaka mmoja kuudhibiti na kuutokomeza ugonjwa huu.”
Kwa mujibu wa takwimu za serikali zilizotolewa Jumatatu, idadi ya visa vilivyothibitishwa vya Ebola nchini DRC imeongezeka hadi 808, ikiwemo vifo 192.
Ripoti ya hali ya ugonjwa huo imebainisha kuwa hadi kufikia Jumapili kulikuwa na visa vipya 26 na vifo vipya 11 vilivyorekodiwa ndani ya saa 24 zilizotangulia.
Wakati huo huo, Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limeonya kuwa fursa ya kuudhibiti mlipuko huo inaendelea kuwa finyu. Mlipuko mbaya zaidi wa Ebola uliwahi kushuhudiwa Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014 na 2016, ambapo zaidi ya watu 11,000 walipoteza maisha.
Frederic Lai Manantsoa, Mratibu wa Dharura wa MSF nchini DRC, amesema: “Huduma za uchunguzi wa maabara, ufuatiliaji wa maambukizi, upatikanaji wa matibabu, pamoja na ushirikishwaji wa jamii, lazima viimarishwe kwa dharura.”
Idadi kubwa ya visa imeripotiwa katika jimbo la Ituri, mashariki mwa DRC. Hata hivyo, maambukizi pia yamebainika katika maeneo mengine ya nchi, pamoja na kuripotiwa kwa visa katika nchi jirani ya Uganda. Mlipuko huu unatofautiana na milipuko ya awali ya Ebola kwani aina ya virusi vya mlipuko huu ni Bundibugyo ambavyo ni nadra. Aidha, hakuna chanjo wala tiba iliyoidhinishwa mahsusi kwa aina hii ya Ebola, ingawa tafiti na majaribio ya chanjo yanaendelea.
Vilevile, mlipuko huu haukutambuliwa kwa wakati, hali iliyoruhusu kusambaa kwake kwa kasi ya kutisha. Kwa sasa, mlipuko wa Ebola unaoikumba DRC tayari umeorodheshwa kuwa wa tatu kwa ukubwa katika historia ya ugonjwa huo.