EU yaonya uwezekano wa kutokea machafuko ya uchaguzi nchini Kenya
Umoja wa Ulaya umeonya kuhusu uwezekano wa kutokea machafuko ya uchaguzi nchini Kenya na kusema kuwa, umetuma timu yake ya kwanza ya wasimamiaji wa uchaguzi nchini humo.
Mkuu wa timu hiyo ya kwanza ya Umoja wa Ulaya ya kusimamia uchaguzi wa Kenya, Marietje Schaake, amesema leo kuwa, timu hiyo ina watu 30 na wametumwa katika maeneo tofauti ya Kenya.
Ameongeza kuwa, maafisa wengine 100 wa kusimamia uchaguzi wa Umoja wa Ulaya watatumwa nchini Kenya wakati wa kukaribia uchaguzi huo. Afisa huyo wa Umoja wa Ulaya amegusia machafuko ya baada ya uchaguzi yaliyoikumbwa Kenya mwaka 2008 na kutaka kuchukuliwa hatua madhubuti za kuzuia kutokea tena machafuko kama hayo.
Uchaguzi Mkuu nchini Kenya unatarajiwa kufanyika tarehe 8 mwezi ujao wa Agosti na kuna mchuano mkali baina ya wagombea wawili, Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee na Raila Odinga wa chama cha ODM ambaye atapeperusha bendera ya muungano wa NASA katika uchaguzi huo.
Hivi karibuni Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya IEBC ilisimamisha kampeni za uchaguzi katika Kaunti ya Siaya baada ya kutokea machafuko baina ya wafuasi wa chama cha Raila Odinga cha ODM.
Machafuko hayo yaliyozimwa haraka na askari wa Kenya yalitokea baina ya wafuasi wa wagombea wa ODM walioteuliwa na chama hicho kugombea na wale wale wa wagombea huru ambao walishindwa katika mchujo wa ODM.
Hadi hivi sasa Raila Odinga ameshagombea katika chaguzi tatu za rais nchini Kenya katika miaka ya 1997, 2007 na 2013. Uchaguzi wa mwaka huu unatajwa kuwa wa mwisho kwa Raila Odinga kugombea.