Mar 16, 2016 03:22 UTC
  • UNICEF yatahadharisha kuhusu hatari ya njaa na utapiamlo inayoikabili Zimbabwe

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kushughulikia Watoto (UNICEF) umetahadharisha juu ya hali mbaya ya njaa nchini Zimbabwe na kutangaza kuwa endapo hatua za lazima hazitochukuliwa juu ya suala hilo baa la njaa na utapiamlo vitavuka kiwango cha kuweza kudhibitika.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Zimbabwe Jane Muita amesema nchi hiyo inakabiliwa na hali mbaya zaidi ya utapiamlo kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 15 iliyopita na kwamba hivi sasa watoto 33,000 wanahitajia huduma za haraka za tiba kutokana na hali mbaya ya utapiamlo waliyonayo. Hayo yanajiri huku serikali ya Harare ikitangaza kuwa watu milioni nne wanahitajia msaada wa chakula.

Katika taarifa aliyotoa kuhusiana na suala hilo, mwakilishi huyo wa UNICEF nchini Zimbabwe ameongeza kuwa japokuwa serikali na asasi mbalimbali zimefanya jitihada kubwa za kutatua tatizo hilo lakini hatua zaidi zinahitajika ili kuweza kulipatia utatuzi kamili.

Kwa mujibu wa msemaji wa UNICEF nchini Zimbabwe Victor Chinyama, kupungua mazao ya kilimo mwaka huu kumeshadidisha hali mbaya ya uhaba wa chakula, njaa na utapiamlo nchini humo.

UNICEF imeomba msaada wa dola milioni 21 ili kuweza kukidhi mahitaji ya watoto nchini Zimbabwe. Mnamo mwezi uliopita, nayo serikali ya Harare iliomba msaada wa dola bilioni moja na milioni 600 kwa ajili ya kununua nafaka na bidhaa nyengine za chakula zinazohitajika.../

Tags