Alkhamisi, Disemba 11, 2025
Leo ni Alkhamisi 20 Mfunguo Tisa Jumadithani 1447 Hijria sawa na Disemba 11 mwaka 2025 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1455 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Bibi Fatima Zahra, binti mtukufu wa Mtume Muhammad (saw).
Bibi Fatima Zahra alilelewa katika nyumba ya wahyi na chini ya malezi bora na mwongozo wa baba yake Mtume Muhammad (saw) na hivyo kuweza kufikia daraja za juu za ukamilifu.
Bibi Fatima (as) alikuwa na nafasi kubwa katika kukabiliana na matatizo na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikimkabili baba yake kutoka kwa washirikina. Mwaka wa pili Hijiria, Bibi Fatima Zahra alifunga ndoa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) ambaye ni dhihirisho la haki, uadilifu na uchaji-Mungu katika sherehe ndogo iliyosimamiwa na Mtukufu Mtume Muhammad (saw).
Vilevile Bibi Fatima akiwa na Imam Ali alifanikiwa kulea shakhsia adhimu kama Hassan, Hussein na Bibi Zainab (as). Mbali na majukumu ya kulea familia, Bibi Fatima Zahra, alijishughulisha pia na malezi ya jamii.

Katika siku kama ya leo miaka 215 iliyopita Alfred Louis Charles de Musset-Pathay malenga na mwandishi mwashuhuri wa Ufaransa alizaliwa katika familiayenye kuzingatia misingi ya utamaduni mjini Paris, Ufaransa.
Musset akiwa na umri wa miaka 19 aliandika diwani yake ya kwanza ya mashairi kwa jina la Simulizi za Uhispania na Italia na hivyo kupata umashuhuri mkubwa kutokana na mbinu yake mpya ya uandishi na hivyo akapata hadhi katika jamii ya mabingwa wa fasihi Ufaransa.
Akiwa na umri wa miaka 22 aliandika tamthilia yake ya kwanza iliyoibua utata kutokana na masuala ya umaanawi na maadili. Fikra zake huru zilipelekea awe miongoni mwa waandishi waatajika wa nusu ya kwanza ya karen ya 19. Alfred de Musset aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 47 mwaka 1857.

Tarehe 11 Disemba miaka 182 iliyopita alizaliwa daktari na mtaalamu wa vividudu maradhi wa Kijerumani aliyevumbua ugonjwa wa kifua kikuu, Robert Koch.
Baada ya kukamilisha masomo katika taaluma ya tiba, Robert Koch alijishughulisha na kutiwa wagonjwa katika miji mbalimbali ya Ujerumani sambamba na kufanya uhakiki kuhusu maradhi tofauti. Tarehe 24 Machi mwaka 1882 alifanikiwa kuvumbua ugonjwa wa kifua kikuu (TB).
Katika safari zake nyingi barani Afrika, tabibu huyo wa Kijerumani pia alibaini kuwa ugonjwa wa malale uliokuwa ukisababisha vifo vya Waafrika wengi ulikuwa ukisababishwa na mdudu anayeitwa mbung'o.

Miaka 127 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria alizaliwa huko Khomein Ayatullahil-Udhmaa Sayyid Ruhullah al-Musawi Khomeini, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Baba yake Imam Khomeini ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu aliuawa shahidi Imam akiwa bado mtoto na hivyo akalelewa na mama na shangazi yake. Baada ya kukamilisha masomo ya msingi Ruhullah Khomeini alijiunga na masomo ya juu kwa walimu mashuhuri hususan Ayatullah Abdul-Karim Hairi na Muhammad Ali Shahabadi. Imam Khomeini alianzisha harakati kubwa zaidi za kupambana na utawala wa kidhalimu wa Shah baada ya kufariki dunia Ayatullah Borujerdi. Upinzani na mapambano yake yalimfanya mtawala kibaraka, Shah ampeleke uhamishoni katika nchi za Uturuki, Iraq na Ufaransa.
Imam aliendeleza mapambano yake dhidi ya Shah akiwa uhamishoni alikobakia kwa kipindi cha karibu miaka 15 na baadaye alirejea nchini na kuuondoa madarakani utawala wa kifalme wa Shah na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapo mwaka 1979.

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita yaani mwaka 1946, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) uliasisiwa baada ya kupasishwa suala hilo kwa wingi wa kura.
Kwa utaratibu huo, taasisi hiyo ikaanza rasmi shughuli zake chini ya Baraza la Masuala ya Kijamii la Umoja wa Mataifa. Awali Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF), ulikuwa na jukumu la kuwahudumia watoto waliojeruhiwa katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Hata hivyo baadaye asasi hiyo muhimu ikapanua zaidi shughuli zake na kuanza kuandaa mahitaji ya kimsingi maishani kama chakula, elimu na malezi kwa watoto waliokosa haki hizo za kimsingi. Makao makuu ya UNICEF yapo mjini New York, Marekani.

Siku kama ya leo yaani tarehe 11 Disemba mwaka 1958 Burkina Faso ilitangazwa kuwa Jamhuri.
Tangu mwanzoni mwa karne ya 19 nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala na ukoloni wa Ufaransa. Burkina Faso ambayo hapo kabla ilikuwa ikiitwa Upper Volta, mnamo mwaka 1958 ilijitangazia utawala wa ndani wa jamhuri. Hata hivyo iliendelea kuwa sehemu ya Ufaransa. Miaka miwili baadaye yaani tarehe 5 Agosti 1960, Burkina Faso ilijipatia uhuru kamili sambamba na kukubaliwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
Mwaka 1984 jina la nchi hiyo lilibadilishwa rasmi kutoka Upper Volta na kuitwa Burkina Faso. Nchi ya Burkina Faso ina ukubwa wa karibu kilomita mraba 274,000 na inapatikana Magharibi mwa Afrika ikipakana na nchi za Mali, Ivory Coast, Ghana, Togo, Benin na Niger.
