Rais Mugabe wa Zimbabwe aelekea Singapore kupata matibabu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31560-rais_mugabe_wa_zimbabwe_aelekea_singapore_kupata_matibabu
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe yuko nchini Singapore kwa ajili ya matibabu, hii ikiwa ni safari yake ya tatu ya kitiba nchini humo mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 09, 2017 23:28 UTC
  • Rais Mugabe wa Zimbabwe aelekea Singapore kupata matibabu

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe yuko nchini Singapore kwa ajili ya matibabu, hii ikiwa ni safari yake ya tatu ya kitiba nchini humo mwaka huu.

Mugabe, ambaye ni kiongozi mkongwe zaidi Afrika akiwa na umri wa miaka 93, alikuwa Singapore mara ya mwisho mwezi Mei na wakati huo msemaji wake, George Charamba, alisema alifika nchini humo kwa ajili ya matibabu ya macho.

Taarifa zinasema Mugabe aliondoka Harare Ijumaa na kuelekea Singapore kwa ajili ya matibabu. Waziri wa Habari Zimbabwe Chris Mushohowe amethibitisha kuwa Mugabe yuko Singapore lakini hakutoa maelezo zaidi.

Rais Mugabe akihutubua mkutano wa Umoja wa Afrika

Chama tawala cha ZANU-PF Jumamosi kiliahirisha mkutano wa vijana uliokuwa umepengwa kufanyika Julai 14 na kuhudhuriwa na rais Mugabe na sababu imetajwa kuwa ni rais huyo kutokuwa ndani ya nchi.

Pamoja na kuwepo wasiwasi kuhusu hali yake ya afya, Mugabe amesafiri mara 10 nje ya nchi mwaka huu na safari yake ya mwisho ya kikazi ilikuwa wiki iliyopita wakati alipohudhuria kikao cha viongozi wa Afrika huko Addis Ababa Ethiopia. Mugabe ambaye ameitawala Zimbabwe tokea ijinyakulie uhuru kutoka Uingereza mwaka 1980 anasema atagombea tena urais mwaka 2018.