UN yataka waliofanya mauaji katikati mwa DRC wasakwe, wakamatwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31718-un_yataka_waliofanya_mauaji_katikati_mwa_drc_wasakwe_wakamatwe
Mkuu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametaka wale wote waliofanya machafuko na mauaji katikati mwa nchi hiyo, wasakwe na kutiwa mbaroni hata kama ni wakuu wa kijeshi na kisiasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 13, 2017 09:47 UTC
  • UN yataka waliofanya mauaji katikati mwa DRC wasakwe, wakamatwe

Mkuu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametaka wale wote waliofanya machafuko na mauaji katikati mwa nchi hiyo, wasakwe na kutiwa mbaroni hata kama ni wakuu wa kijeshi na kisiasa.

José Maria Aranaz amesema hayo leo Alkhamisi na kuongeza kuwa, uchunguzi wa kuwagundua waliofanya machafuko na mauaji katika eneo la Kasai la katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unapaswa ufanywe haraka hasa baada ya kugunduliwa makaburi 80 ya umati. Amesema, kuna udharura wa kutiwa mbaroni hata viongozi wa kijeshi na kisiasa waliohusika na mauaji hayo.

Jana Jumatano Umoja wa Mataifa ulitangaza kugunduliwa makaburi mengine 38 ya umati katika eneo la Kasai na hivyo kufanya idadi ya makaburi ya umati yaliyogunduliwa na umoja huo huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufikia 80.

Moja ya makaburi ya umati Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

 

Vile vile José Maria Aranaz ametaka kukomeshwa mara moja mauaji katika eneo la Kasai ambalo kwa miezi tisa sasa linashuhudia machafuko na mapigano baina ya jeshi la serikali na waasi.

Jana, ofisi ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilitangaza kuwa, makaburi hayo 38 ya umati yamegunduliwa katika maeneo sita tofauti kwenye operesheni ya pamoja kati yao na maafisa wa uchunguzi wa jeshi la Congo katika eneo la magharibi mwa Kasai.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Kanisa Katoliki, zaidi ya watu elfu tatu wameshauawa katika machafuko na mapigano kwenye eneo hilo la Kasai na takriban watu milioni moja na laki tatu wamekimbia maeneo yao na wengine kukimbilia katika nchi jirani ya Angola.