Kenya na Iran zaafikiana kutotoza ushuru mara mbili
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Kenya zimetiliana saini mapatano ya kutotozana ushuru mara mbili na pia kuzuia watu au mashirika ya nchi mbili kukwepa kulipa ushuru unaotokana na mapato na uwekezaji.
Kwa mujibu wa Shirika la Ustawi wa Biashara Iran, Murtadha Daylan, Mwambata wa Kibiashara katika Ubalozi wa Iran nchini Kenya, mapatano hayo yamefikiwa katika kikao kilichohudhuriwa na Hadi Farajvand Balozi wa Iran nchini Kenya na Katibu Katika Wizara ya Fedha Dkt Kamau Thugge.
Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Farajvand ameitaja Kenya kuwa lango la kuingia eneo la Afrika Mashariki huku Iran ikiwa ni lango la kuingia nchi za Urusi ya zamani maarufu kama CIS na nchi zingine za eneo hilo. Amesema Kenya ni mshirika wa kuaminika wa kibiashara na kiuchumi.
Katika kikao hicho Kamau Thugge ameashiria udharura wa kuangaliwa upya na kuimarishwa uwezo wa Iran na Kenya katika sekta za kilimo, viwanda na biashara na ameitaka Iran iipe Kenya uzoefu wake katika sekta mbali mbali.
Aidha ameongeza kuwa, kufikiwa mapatano hayo ya ushuru kutapelekea kuongezeka wawekezaji na kuimarishwa kiwango cha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya pande mbili.
Hivi karibuni mwambata wa kibiashara wa Iran mjini Nairobi alisema Kenya inaongoza katika ununuzi wa bidhaa kutoka Iran barani Afrika na ni ya 15 kwa ujumla katika ununuzi wa bidhaa za Iran duniani.
Aliongeza kuwa kwa ujumla Kenya ni nchi ya 15 yenye kununua bidhaa kutoka Iran kwa mujibu wa takwimu za mwezi Machi mwaka 2017.