Jul 25, 2017 02:59 UTC
  • UN yaitaka serikali ya Nigeria kuwakomboa wasichana wa Chibok

Kamati ya Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa imeitaka serikali ya Nigeria kuzidisha juhudi za kuwakomboa wanawake na wasichana wote waliotekwa nyara na kundi la Boko Haram na kuhakikisha wanarudi shuleni bila ya kukabiliwa na unyanyapaa.

Taarifa iliyotolewa na kundi la wataalamu 23 wa Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema: Nigeria inapaswa "kuimarisha jitihada zake za kuwaokoa wanawake na wasichana wote waliochukuliwa mateka na waasi wa Boko Haram, kuwaingiza katika mchakato wa kuwarejesha katika jamii na kuwapa wao na familia zao, huduma za kisaikolojia na nyingine za matibabu.

Taarifa ya kundi hilo imesema, wanawake na wasichana waliotekwa nyara na Boko Haram kutoka Chibok na Damasak katika Jimbo la Borno Aprili mwaka 2014 wanaendelea kunajisiwa, kufanywa watumwa wa ngono, kulazimishwa kuolewa na kutiwa mimba na waasi wa Boko Haram.

Baadhi ya wasichana wa Shule ya Chibok waliotoroka au kukombolewa kutoka kwa Boko Haram

Wasichana wasiopungua 100 kati ya wanafunzi 270 wa Shule ya Chibok waliochukuliwa mateka na kundi la Boko Haram mwaka 2014 wangali wanashikiliwa na kundi hilo kama watumwa wa ngono. Wasichana wengine 100 wameachiwa huru na 60 wamefanikiwa kutoroka.  

Tags