Makundi ya waasi yazidi kuchipuka mashariki mwa Kongo DR
(last modified Fri, 18 Mar 2016 03:00:40 GMT )
Mar 18, 2016 03:00 UTC
  • Makundi ya waasi yazidi kuchipuka mashariki mwa Kongo DR

Asasi za kiraia huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, zimetangaza kuweko ongezeko kubwa la makundi ya waasi katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa asasi hizo, eneo la mashariki mwa nchi hiyo limekuwa ngome ya makundi ya waasi kiasi cha kuwanyima amani wakazi wa maeneo hayo. Ripoti hiyo imetolewa kufuatia kuonekana waasi kadhaa wa kundi linalojiita Raïa Mutomboki katika eneo la Kalehe ndani ya mkoa wa Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Aidha duru za kiraia zimeongeza kuwa, wanamgambo wa kundi hilo wamejizatiti kwa zana za kijeshi ikiwemo bunduki. Kwa mujibu wa watu walioshuhudia, wanamgambo wengine kadhaa wa kundi hilo la waasi wako katika maeneo ya Kanyanja, Ngamba na Muzimu. Inaelezwa kuwa siku ya Jumanne waasi hao walivamia na kupora mali za wakazi wa mji wa Ngamba. Wakazi wa maeneo hayo wamelitaka jeshi la serikali kufanya operesheni kali dhidi ya waasi hao ili kurejesha usalama kwa wakazi wa maeneo hayo.