Gambia na Senegal kushirikiana katika vita dhidi ya ugaidi
Mawaziri wa Mambo ya Ndani wa nchi za Senegal na Gambia wametilia mkazo umuhimu wa kushirikiana nchi zao katika vita dhidi ya ugaidi.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Senegal, Abdoulaye Daouda Diallo na mwenzake wa Gambia, Mai Ahmad Fatty walikutana jana Jumanne huko Dakar, mji mkuu wa Senegal na kujadiliana njia za kuimarisha uhusiano wa pande mbili na kupambana na ugaidi na misimamo mikali.

Mawaziri wa Mambo ya Ndani wa Gambia na Senegal wamezungumzia pia mapambano dhidi ya magendo ya madawa ya kulevya hususan katika mpaka wa nchi hizo mbili na wajibu wa kuongeza ushirikiano wao katika jambo hilo.
Ikumbukwe kuwa, wakati wa urais wa Yahya Jammeh nchini Gambia, nchi hiyo haikuwa na uhusiano mzuri na jirani yake Senegal.
Hivi sasa Senegal iko mstari wa mbele katika juhudi za kuirejea Gambia katika hali ya kawaida ya kisiasa baada ya kutokea mgogoro wa kisiasa wa baada ya uchaguzi mkuu uliofuatiwa na Yahya Jammeh kukataa kushindwa na baadaye kulazimika kuikimbia nchi.