Mlipuko nadra wa homa ya Bonde la Ufa wauwa watu 17 Senegal
Mamlaka za afya nchini Senegal zimethibitisha kuaga dunia watu 17 katika kile kinachoelezwa kuwa mlipuko mkubwa wa Homa ya Bonde la Ufa (RVF). Mlipuko huu wa homa ya Bonde la Ufa umetajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kuiathiri Senegal katika miongo kadhaa.
Dakta Boly Diop Mkuu wa uchunguzi wa homa ya Bonde la Ufa (RVF) katika Wizara ya Afya ya Senegal ameeleza kuwa watu119 wamesajiliwa kupatwa na homa hiyo tangu kutangazwa kwa mlipuko wa ugonjwa huo Septemba 21 mwaka huu; wagonjwa wengi wakiripotiwa katika maeneo ya kaskazini yanayojishughulisha na ufugaji.
"Hii ni mara ya kwanza Senegal ambapo idadi kubwa ya watu imekumbwa na maradhi hayo," amesema Dakta Boly Diop.
Homa ya Bonde la Ufa ni ugonjwa unaoenezwa na mbu ambao huathiri mifugo kama vile ng'ombe, mbuzi na kondoo. Wanadamu wanaweza kuambukizwa kupitia kuumwa na mbu au kugusana na wanyama walioambukizwa, hasa wakati wa kuchinja au kujifungua.
Maambukizi makali ya homa ya Bonde la Ufa yanaweza kusababisha kuvimba kwa ubongo, kupofuka macho au homa ya kuvuja damu, hali ambazo zinaweza kusababisha kifo.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuwa wafugaji, wakulima, na wafanyakazi wa machinjio ya mifugo wako katika hatari kubwa ya kupatwa na maambukizi.