Je, umewadia sasa wakati wa kuhitimishwa ukoloni wa Ufaransa barani Afrika?
Ufaransa imehitimisha muda wa zaidi ya miaka sitini ya uwepo wake wa kudumu wa kijeshi nchini Senegal kwa kukabidhi kambi ya kijeshi ya Geille iliyoko mjini Dakar kwa jeshi la nchi hiyo.
Kambi hiyo, iliyokuwa kambi kubwa zaidi na ya mwisho ya Ufaransa magharibi mwa Afrika, ilikuwa na ukubwa wa hekta tano na ilionekana kama nembo ya ushawishi wa kijeshi wa Ufaransa tangu enzi ya ukoloni. Kwa maana hiyo, kukabidhiwa Senegal kambi ya Geille ni ishara yenye maana kubwa ya kujiri mabadiliko makubwa na ya kina katika uhusiano wa kisiasa, kijamii na kiuchumi kati ya Afrika na Ufaransa na kufikia tamati zama za utegemezi wa Afrika kwa madola ya kikoloni.
Kuondoka wanajeshi wa Ufaransa barani Afrika, ambako kumeshtadi katika miaka ya hivi karibuni, inapasa kuchukuliwe kama nukta ya mabadiliko makubwa katika historia ya matukio ya bara la Afrika; mabadiliko ambayo yameibuka kutokana na upinzani wa miaka mingi, mabadiliko ya kisiasa na kijamii, na kuongezeka matakwa ya watu wa bara hilo.
Ukweli ni kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, nchi mbalimbali za Kiafrika, zikiwemo Mali, Niger, na Burkina Faso, zimepaza sauti kutaka Ufaransa iondoke katika ardhi zao na kukomeshwa uwepo wa jeshi la Ufaransa katika nchi hizo. Mchakato huo ulioanzia nchini Mali, sasa umefikia kilele kwa kuondolewa rasmi vikosi vya Ufaransa nchini Senegal; uondokaji ambao sio tu unaashiria kumalizika zama za uwepo wa moja kwa moja wa kijeshi wa Ufaransa huko Magharibi na Katikati mwa Afrika, lakini pia ni nembo ya kuhitimishwa kipindi kirefu cha satua na ushawishi wa kikoloni, ambao chimbuko lake ni historia chafu na ya giza ya ukoloni.
Ufaransa, ambayo katika karne ya 19 na 20, ikiwa moja ya madola makubwa ya kikoloni ilidhibiti na kuhodhi sehemu kubwa ya ardhi ya bara la Afrika, ilijinufaisha bila ya kiwango wala mpaka na maliasili na rasilimaliwatu za nchi za bara hilo; kiasi kwamba, sio tu ilikuwa na nafasi kubwa katika kusarifu miundo ya kiuchumi na kisiasa ya nchi hizo kulingana na maslahi yake, lakini pia ilikuwa na nafasi isiyosahaulika katika mauaji, udhalilishaji na unyanyasaji wa kikatili uliofanywa katika nchi hizo ambao kumbukumbu zake zimesalia katika historia.
Nchi nyingi za Kiafrika hazitasahau uchokozi na vitendo vya kikatili vilivyofanywa na Ufaransa wakati wa enzi za ukoloni. Kama historia ya Algeria

inavyoonyesha, katika nchi hiyo Ufaransa sio tu ilinyakua ardhi na kupora rasilimali, lakini pia ilifanya ukandamizaji mkubwa na wa kikatili dhidi ya mapambano na upinzani wa wananchi ulioteketeza roho za mamilioni ya watu mbali na iliowapeleka uhamishoni. Majaribio ya nyuklia ambayo Ufaransa ilifanya kwa kuwatumia Waalgeria ni hatua nyingine ya kinyama ambayo haitafutika katika kumbukumbu za watu wa nchi hiyo. Matukio hayo yameacha kumbukumbu nzito na chungu katika fikra za watu Waafrika ambayo imerithishwa kutoka kizazi hadi kizazi na kuwa nafasi muhimu leo hii katika kujenga utambulisho wao wa kisiasa na kitaifa.
Japokuwa baada ya nchi za Afrika kujipatia uhuru wao, katika miongo ya katikati ya karne ya ishirini Ufaransa iliendelea kudumisha uwepo wake mkubwa wa kijeshi katika eneo hilo kwa kisingizio cha kudumisha amani na kulinda usalama, na vikosi vya jeshi la Ufaransa vikasambazwa katika nchi mbali mbali za Kiafrika kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, kudumisha utulivu, na kufanya operesheni za pamoja na majeshi ya nchi hizo, lakini uwepo huo pia haukukubaliwa na nchi hizo; na wananchi wa mataifa hayo wakauchukulia kuwa ni nembo ya kuendelezwa satua ya kikoloni na utegemezi wa kisiasa. Unyonyaji uliofanywa na Ufaransa wa maliasili zenye utajiri mkubwa za nchi za Afrika kama vile mafuta, gesi, urani na migodi ya dhahabu na almasi, pamoja na utekelezaji wa sera onevu za kiuchumi ambazo mara nyingi zilinufaisha makampuni ya Ufaransa na kuwaumiza wenyeji, kulizidisha wimbi la manung’uniko ya umma.
Kwa upande mwingine, katika miaka ya karibuni, kutokana na kubadilika hali ya kisiasa na kiuchumi katika nchi mbalimbali, kupatikana maendeleo ya kiteknolojia na wigo mpana wa mawasiliano, nchi nyingi za Kiafrika nazo pia zimepata maendeleo mengi ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. Maendeleo hayo, hasa katika miongo ya karibuni, yamepelekea matakwa ya umma kuvuka mipaka ya utegemezi wa kihistoria na kijeshi tu. Hivi sasa, akthari ya serikali na wananchi wa mataifa ya Afrika yanataka uhuru wa kweli wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni na hawako tayari kutawaliwa tena na madola ya kigeni ikiwemo Ufaransa kupitia utegemezi wa kijeshi na kisiasa.
Taasisi ya Sera ya Kimataifa ya Austria imeeleza yafuatayo katika uchambuzi wake juu ya suala hilo: “hatua ya nchi za Kiafrika ya kuwafukuza wanajeshi wa Ufaransa ni sehemu ya mchakato mpana wa kupigania kuwa huru na kutilia mkazo mamlaka ya kitaifa ya kujitawala; na hilo linaweza kutajwa kama wimbi la pili la kutokomeza ukoloni barani Afrika”…/