Aug 30, 2017 07:36 UTC
  • Boko Haram waendelea kuwateka nyara raia kaskazini mashariki mwa Nigeria

Kundi la kigaidi la Boko Haram limeendelea kuhatarisha maisha ya raia kaskazini mashariki mwa Nigeria baada ya kuwateka nyara watu kadhaa wa familia moja.

Ripoti zinasema kuwa, wanamgambo wa Boko Haram wamewateka nyara watu wa familia moja jirani na Dikwa huko Maiduguri kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuzusha hofu kubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo. 

Taarifa za awali zinasema kuwa, watu tisa wa familia moja walitekwa nyara na wanamgambo wa Boko Haram wakati walipokuwa katika barabara kuu ya Maiduguri-Gubio wakisubiri usafiri. Hayo yameelezwa na mmoja wa wanafamilia hao ambaye anashiriki katika vita dhidi ya Boko Haram.

Miongoni mwa waliotekwa nyara ni mwanamke mmoja, mabinti wake watatu pamoja na dada yake.

Raia wa Chad waliolazimika kuwa wakimbizi baada ya kuongezeka mashambulio ya Boko Haram katika Bonde la Ziwa Chad

Wakati wanamgambo wa Boko Haram wakiendelea na utekaji nyara hasa katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria, imeelezwa kuwa, Rais Muhamadu Buhari amekuwa akipatiwa taarifa zisizo sahihi kuhusiana na uwezo hasa wa kundi hilo la kigaidi.

Zaidi ya watu 20,000 wameuawa hadi sasa na wengine wapatao milioni mbili na laki saba wamebaki bila makaazi tangu kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram lilipoanzisha uasi na mashambulio nchini Nigeria kwa lengo la eti kuunda dola la Khilafa.

Wigo wa mashambulio ya kundi hilo umepanuka na kuenea eneo zima la Bonde la Ziwa Chad kwa kuvuka mpaka hadi ndani ya ardhi za nchi jirani za Cameroon, Niger na Chad.

Tags