Sudan Kusini yaondoa majeshi yake katika mpaka na jirani yake Sudan
Serikali ya Sudan Kusini imetangaza kuwa, imetekeleza amri ya kuondoa vikosi vyake vya jeshi katika mpaka wa nchi hiyo na jirani yake, Sudan.
Afisa wa ngazi za juu wa Sudan Kusini ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema kuwa, jeshi la nchi hiyo limetii amri ya Rais Salva Kiir ya kuondoa majeshi ya nchi hiyo katika mipaka ya pamoja na jirani yake, Sudan kwa shabaha ya kutekeleza mpango wa kurejesha uhusiano wa kawaida baina ya nchi mbili hizo majirani.
Hatua hiyo ya Sudan Kusini imechukuliwa sambamba na tishio la Sudan ambayo ilitangaza kuwa, itachukua maamuzi ya kufunga mipaka yake na jirani yake huyo endapo Sudan Kusini itaunga mkono harakati za waasi wa Darfur katika maeneo mawili ya Kordofan Kusini na Blue Nile.
Serikali ya Khartoum inadai kuwa, serikali ya Juba inaendelea kuyaunga mkono makundi ya waasi yanayofanya uhalifu katika eneo la Darfur. Aidha serikali ya Khartoum inadai kuwa makundi hayo ya waasi yamekuwa yakifanya jinai za kutisha katika majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile. Hata hivyo serikali ya Juba imekuwa ikipuuzilia mbali madai hayo.
Januari mwaka huu, al-Bashir aliagiza kufunguliwa mpaka wa nchi yake na Sudan Kusini kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2011, baada ya eneo hilo kujitenga rasmi na kujitangazia uhuru.