Upinzani Afrika Kusini waanzisha jitihada mpya za kumuuzulu Zuma
Vyama vya upinzani nchini Afrika Kusini vimeanzisha jitihada mpya za kumuondoa madarakani Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo ambaye tayari anaandamwa na kesi chungu nzima za ufisadi na utumiaji mbaya wa mamlaka.
Vyama hivyo jana Jumanne viliitaka Mahakama ya Katiba mjini Johannesburg kuliagiza Bunge la nchi hiyo lianzishe uchunguzi dhidi ya Zuma kwa madai ya ufisadi yanayomkabili na hususan madai ya kutumia mamilioni ya dola, fedha za umma kukarabati nyumba yake binafsi katika eneo la Nkandla, KwaZulu-Natal, kitendo ambacho wanadai kuwa kinakiuka katiba.
Zuma ameponea mara kadhaa kuondolewa madarakani kupitia Bunge la nchi hiyo. Mwezi uliopita, Zuma alinusurika kuenguliwa madarakani baada ya kupataka uungaji mkono hafifu wa chama tawala ANC katika kura ya kutokuwa na imani naye Bungeni.
Hiyo ilikuwa ni mara ya nane kwa Rais Zuma kunusurika na shoka hilo la Bunge.
Mawakili wa vyama hivyo vya upinzani Afrika Kusini wakiongozwa na Tembeka Ngcukaitobi wameiambia Mahakama ya Katiba kuwa, kuna haja ya kuchunguzwa mienendo ya Zuma kwa kuwa anaandamwa na kesi zaidi ya 800 za rushwa na kwa msingi huo hastahili kuendelea kuiongoza nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
Wananchi wa Afrika Kusini wamekuwa wakifanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi wakitaka kiongozi huyo ajiuzulu, hatua ambayo hadi sasa imeshindwa kuzaa matunda.