Juhudi za wapinzani wa serikali Afrika Kusini za kumuondoa madarakani Jacob Zuma
Vyama vya upinzani nchini Afrika Kusini vimeanzisha mikakati mipya ya kumsaili na kumuondoa madarakani Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma kwa kuwasilisha mashtaka katika Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo.
Katika mashtaka hayo, vyama vya upinzani nchini Afrika Kusini vimemtaka Spika wa Bunge, Baleka Mbete aitishe kikao cha Bunge cha kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais Jacob Zuma kwa kutegemea nyaraka na ushahidi uliowasilishwa mahakamani. Vilevile vimelitaka Bunge kufanya uchunguzi kuhusu mali na milki za Zuma hususan nyumba na makazi yake binafsi.
Mivutano ya kisiasa kati ya Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini na vyama vya upinzani inaendelea kwa muda sasa. Vyama hivyo vinamtuhumu Zuma kwamba ametumia vibaya fedha za umma kwa maslahi yake binafsi na kukarabati nyumba yake. Japokuwa Rais wa Afrika Kusini ameomba radhi na kurejesha fedha hizo katika hazina ya dola, lakini wapinzani wake wanasema kuwa, serikali yake imezama kwenye ufisadi na wanasisitiza kuwa, kuna ulazima wa kupambana na uozo huo.
Siku chache zilizopita pia Cyril Ramaphosa ambaye ni miongoni mwa wanaowania kurithi nafasi ya Zuma katika chama tawala cha ANC alitoa wito wa kuundwa kamisheni huru ya kufuatilia faili la ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.
Mivutano ya kisiasa nchini Afrika Kusini ilishadidi zaidi baada ya Rais Zuma kumfuta kazi aliyekuwa Waziri wa Fedha wa nchi hiyo, Pravin Gordhan. Wapinzani wanasema kuwa Gordhan amefutwa kazi kwa sababu ya kufichua kashfa ya ufisadi ndani ya serikali ya Jacob Zuma na jitihada zake za kupambana na ubadhirifu. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita Zuma ameokoka majaribio manne ya kumuuzulu bungeni lakini suala hilo halijapunguza malalamiko ya kambi ya upinzani dhidi ya kiongozi huyo. Chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) kinasisitiza kuwa, kitaendeleza jitihada za kisheria ikiwa ni pamoja na maandamano na mikusanyiko ya malalamiko dhidi ya Zuma hadi kiongozi huyo atakapoondolewa madarakani.
Hii ni pamoja na kuwa, Afrika Kusini ambayo inahesabiwa kuwa miongoni mwa nguvu kubwa za kiuchumi barani Afrika inasumbuliwa na tatizo la kupungua ustawi wa kiuchumi na ongezeko la umaskini na ukosefu wa ajira. Hali hiyo imezidisha misuguano ya kijamii na kisiasa nchini humo sambamba na ukatili na mashambulizi yanayofanywa na raia wa kawaida dhidi ya raia wa nchi za kigeni wanaoishini nchini humo.
Hali hiyo inahatarisha nafasi ya chama tawala cha ANC kinachoongozwa na Jacob Zuma baina ya watu wa Afrika Kusini. Chama hicho ambacho mwaka jana pia kilipata pigo kubwa katika uchaguzi wa mabaraza ya miji, kina wasiwasi wa kupungua zaidi uungaji mkono wa wananchi.
Kwa kuzingatia yote hayo inaonekana kuwa, utendaji wa Rais Jacob Zuma katika kipindi kilichobakia cha uongozi wake utakuwa na nafasi na mchango muhimu katika ushindi au kushindwa chama cha ANC katika uchaguzi mkuu wa 2019.