Sep 23, 2017 15:17 UTC
  • Boko Haram yaua watu 9 katika kambi ya wakimbizi Borno, Nigeria

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram wamewaua watu tisa waliokuwa wakiishi katika kambi ya wakimbizi katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Taarifa iliyotolewa na polisi ya Nigeria imesema kuwa, wanachama wa kundi hilo wamefanya shambulizi hilo karibu na mji wa Ron jimboni hapo.

Wahanga wote wa jinai hiyo walikuwa wakiishi katika kambi ya wakimbizi ya mji huo na baada ya machafuko kupungua na kuanza msimu wa masika waliamua kujishughulisha na kazi ya kilimo.

Abubakar Shekau (katikati), kiongozi wa Boko Haram

Hata hivyo wakati wakiendelea na shughuli yao hiyo, wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram waliwavamia na kuwaua. Kundi la Boko Haram lilianzisha mashambulizi yake nchini Nigeria tangu mwaka 2009 ambapo kuanzia kipindi hicho hadi sasa limeua zaidi ya watu 20,000 katika nchi za Nigeria, Cameroon, Niger na Chad. Zaidi ya watu milioni mbili wamekuwa wakimbizi huku hujuma na mashambulizi ya kundi hilo yakiwa bado yanaendelea. 

Tags