Katibu Mkuu wa UN asisitiza umuhimu wa kutatuliwa migogoro ya Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35663-katibu_mkuu_wa_un_asisitiza_umuhimu_wa_kutatuliwa_migogoro_ya_afrika
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza umuhimu wa kutatuliwa migogoro ya Afrika kwa shabaha ya kutafuta sababu na chanzo cha njaa na uhaba wa chakula katika nchi za bara hilo na huko Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 14, 2017 23:25 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN asisitiza umuhimu wa kutatuliwa migogoro ya Afrika

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza umuhimu wa kutatuliwa migogoro ya Afrika kwa shabaha ya kutafuta sababu na chanzo cha njaa na uhaba wa chakula katika nchi za bara hilo na huko Yemen.

Antonio Guterres ameashiria athari mbaya za ukosefu wa chakula na machafuko ya ndani katika nchi kama Sudan Kusini, Somalia, Nigeria, Yemen na kadhalika na kutahadharisha kuwa, jamii za maneneo hayo zitaendelea kusumbuliwa na njaa na mashaka mengi hadi pale machafuko na migororo hiyo itakapokomeshwa. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa matamshi hiyo wakati nchi nyingi za Afrika na Mashariki ya Kati zikiendelea kusumbuliwa na vita na migogoro mingi. Mbali na kusababisha migogoro ya kisiasa ya kiusalama, machafuko hayo pia yamezidisha njaa na mgogoro wa kibinadamu katika nchi nyingi za bara la Afrika. Chanzo cha baadhi ya machafuko na mapigano yanayojiri katika maeneo hayo kama Sudan Kusini ni mivutano ya ndani na katika maeneo mengine ni madola ya kigeni, makundi ya kigaidi na ya waasi. 

Vita na mapigano ya ndani katika baadhi ya nchi za Afrika vinatokana na hitilafu za kikabila, kidini, muundo wa kijadi wa jamii, umaskini, kubakia nyuma kisiasa na kijamii, kutokuwepo demokrasia, uchumi mbaya na uingiliaji wa madola ya kigeni hususan ya Magharibi katika nchi za bara hilo. 

Hitilafu za kikabilia na kidini ni miongoni mwa sababu za machafuko ya nchi za Afrika

Kwa mfano tu chanzo cha machafuko na mapigano ya miaka kadhaa sasa huko Sudan Kusini ni hitilafu za kikabila zinazosababisha mauaji yanayotajwa kuwa ni mauaji ya kimbari. Hali hiyo pia inashuhudiwa katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Kama tulivyoashiria sehemu nyingine ya migogoro ya sasa ya Afrika na Mashariki ya Kati ni matokeo ya njama za kigeni au sera za madola ya kigeni yanayotaka kudhamini au kulinda maslahi yao kupitia njia hiyo. Vilevile kuna harakati za makundi ya kigaidi kama Boko Haram na al Shabab ambayo nayo pia yanahudumia malengo ya Wamagharibi kwa njia moja au nyingine. Kwa mfano tu harakati za kundi la Boko Haram huko kaskazini mwa Nigeria zimesababisha ukosefu wa chakula na njaa kwa mamilioni ya wakazi wa maeneo hayo ambao wengi wao wameamua kukimbia makazi yao kwa kuhofia kuuawa. Takwimu zinasema zaidi ya watu milioni nane na nusu wa kaskazini mashariki mwa Nigeria wanahitajia misaada ya kibinadamu. Hali kama hiyo au mbaya zaidi pia inaonekana nchini Somalia ambako mamilioni ya watu wanasumbuliwa na njaa, maradhi na umaskini hususan katika maeneo yenye vita na machafuko yaliyosababishwa na uvamizi wa kundi la kigaidi la al Shabab. 

Uvamizi na mashambulizi ya Saudi Arabia dhidi ya taifa la Yemen pia yamesababisha maafa makubwa ikiwa ni pamoja na njaa, maradhi na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya nchi hiyo. Hadi sasa mamia ya raia wasio na hatia wa Yemen wamekuwa wahanga wa ugonjwa wa kipindupindu ambao baadhi ya taasisi za kimataifa zinasisitiza kuwa, unaenezwa na kutumiwa na Saudi Arabia na washirika wake kama silaha ya vita.

Watoto wa Yemen wanaendelea kuuawa katika mashambulizi ya Saudi Arabia

Japokuwa jumuiya na taasisi za kimataifa zimetenga misaada ya aina mbalimbali kwa ajili ya maeneo hayo lakini inaonekana kuwa, misaada hiyo haiwezi kuwaokoa waathiriwa; kwa msingi huo njia ya kukomesha mashaka na kurejeshwa amani katika maeneo hayo ni kukomeshwa kikamilifu migogoro ya kibinadamu, vita na machafuko. Ukweli huu unasisitizwa na Mkuu wa Kamisheni Kuu wa Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa, Filippo Grandi, ambaye amesema kuwa: Njia ya kukomesha migogoro ni kukomeshwa mapigano ya silaha kote duniani.