8 waaga dunia na kujeruhiwa baada ya ndege ya mizigo kuanguka Kodivaa
(last modified Sun, 15 Oct 2017 07:54:32 GMT )
Oct 15, 2017 07:54 UTC
  • 8 waaga dunia na kujeruhiwa baada ya ndege ya mizigo kuanguka Kodivaa

Raia wanne wa Moldova wamepoteza maisha huku wengine wanne wakijeruhiwa baada ya ndege ya mizigo iliyokodishwa na jeshi la Ufaransa kuanguka baharini, karibu na uwanja wa kimataifa wa ndege wa mji mkuu wa Ivory Coast, Abidjan.

Waziri wa Usalama wa Kodivaa, Sidiki Diakite ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, ajali hiyo ilitokea jana Jumamosi na kwamba wanajeshi wa Ufaransa ni miongoni mwa majeruhi.

Naye msemaji wa jeshi la Ufaransa, Kanali Patrick Steiger amesema ndege hiyo imekuwa ikitumika katika operesheni za kilojistiki za kikosi cha Ufaransa cha Barkhane, kinachopambana na magenge ya kigaidi katika eneo la maghairibi mwa Afrika.

Askari wa kikosi cha Barkhane cha Ufaransa nchini Kodivaa

Habari zinasema kuwa, watu kadhaa walionusurika katika ajali hiyo walikimbizwa katika zahanati ya karibu, huku waliokuwa na majeraha madogo wakitibiwa na kuruhusiwa kuondoka. Mashahidi wanasema mabaki ya ndege hiyo aina ya Turboprop yalisombwa hadi katika ufukwe wa bahari hiyo.

Maafisa wa usalama nchini Cote d'Ivoire wanasema yumkini ndege hiyo aina ya Turboprop (Antonov) inayoaminika kutengezewa nchini Ukraine, ilianguka kutokana na  mvua kubwa iliyonyesha hiyo jana karibu na bandari ya Bouet.