Mugabe akataa tena kujiuzulu
Licha ya hapo awali kutangazwa kuwa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amekubali kujiuzulu na kwamba angeliitumia hotuba yake kwa taifa kutangaza rasmi kuachia madaraka, lakini rais huyo kizee hakusema chochote kuhusiana na kujiuluzu kwake wakati alipolihutubia taifa jana usiku.
Mugabe alilihutubia taifa jana usiku kama ilivyotangazwa kabla lakini hakugusia kabisa suala la kujiuzulu urais baada ya kuiongoza Zimbabwe kwa muda wa miaka 37.
Kabla ya hapo, vyombo vya habari vya Zimbabwe vilikuwa vimetangaza jana kwamba Mugabe amekubali kujiuzulu baada ya jeshi kumpa muda wa mwisho wa kubakia madarakani na baada ya kufanyika mazungumzo ya kina kuhusiana na kujiuzulu kwake.
Siku ya Jumatano ya tarehe 15 Novemba, jeshi la Zimbabwe lilitangaza kumuondoa madarakani Rais Robert Mugabe na kumuweka katika kifungo cha nyumbani yeye na familia yake.
Jeshi la Zimbabwe lilichukua hatua hiyo kupinga hatua ya Rais Mugabe ya siku kadhaa za kabla yake ambapo veterani huyo wa vita vya ukombozi wa Zimbabwe alimfuta kazi makamu wake Emmerson Mnangagwa ambaye watu wengi waliamini kuwa angelichukua nafasi ya Mugabe kama Rais na mkuu wa chama tawala cha Zanu-PF.
Inaonekana wazi kwamba Mugabe anataka mke wake Grace Mugabe arithi nafasi yake wakati atakapomaliza muda wake. Kabla ya hapo Mugabe alikuwa amesema atahakikisha anabakia madarakani hadi kipindi chake cha urais kitakapomalizika mwishoni mwa mwaka ujao wa 2018.