Hatimaye Rais Mugabe wa Zimbabwe asalimu amri, akubali kujiuzulu
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe hatimaye amesalimu amri na kukubali kujiuzulu. kufutia mashinikizo ya kila upande ya kumtaka aachie madaraka.
Jacob Mubenda, Spika wa Bunge la Zimbabwe amesema amepokea barua ya kujiuzulu kutoka kwa kiongozi huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 93.
Katika barua hiyo ya kujiuzulu, Mugabe amesema anajiuzulu kwa khiari, ili kupisha mapokezano ya uongozi kwa njia ya amani, baada ya kuiongoza nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kwa karibu miongo minne.
Baada ya Spika wa Bunge la Zimbabwe kutoa tangazo la kujiuzulu kwa Mugabe, wananchi wa taifa hilo wamejitokeza mabarabarani kwa shangwe, nderemo na vifijo kusherehekea habari hizo.
Mapema leo muungano wa maveterani wa vita vya uhuru nchini Zimbabwe ulikuwa umetoa wito wa kufanyika maandamano dhidi ya Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo ili kumshinikiza ajiuzulu na kuachia madaraka ya nchi.
Mkuu wa Muungano wa Maveterani wa Vita nchini Zimbabwe ametaka kufanyika maandamano dhidi ya Mugabe haraka iwezekanavyo na kumshinikiza kiongozi huyo ajiuzulu.
Chris Mutsvangwa amesema leo kuwa, anawataka wananchi wajitokeze kwa wingi katika maandamano ili kumshinikiza Mugabe aliyekaa madarakani kwa muda wa miaka 37 ajiuzulu na kuachia hatamu za uongozi wa nchi.
Wakati huo huo, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Harare mji mkuu wa Zimbabwe wameandamana dhidi ya Mugabe aliye na miaka 93 huku wakipiga nara dhidi ya kiongozi huyo wakimtaka aondoke madarakani. Viongozi wa chuo hicho kikuu cha mjini Harare wamesema kuwa, wameakhirisha mitihani iliyotazamiwa kufanywa chuoni hapo hadi wakati mwingine. Jeshi la Zimbabwe Jumatano tarehe 15 mwezi huu lilitangaza kuwa Mugabe na familia yake wapo katika kifungo cha nyumbani na kisha kumuondoa uongozini.
Jeshi la Zimbabwe lilichukua hatua hiyo kama radiamali kwa hatua ya siku kadhaa zilizopita iliyochukuliwa na Mugabe ya kumuuzulu aliyekuwa Makamu wake Emmerson Mnangagwa ili aweze kumrithisha nafasi hiyo mkewe Bi Grace Mugabe.