Rais mtarajiwa wa Zimbabwe kuapishwa leo
Rais mtarajiwa wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa anatarajiwa kutawazwa leo Ijumaa, ikiwa ni siku tatu tu baada ya mtangulizi wake Robert Mugabe kuachia ngazi kwa mashinikizo ya jeshi na chama chake cha Zanu-PF.
Emmerson Mnangagwa aliyekua makamu wa rais wa Zimbabwe anamrithi Mugabe, baada ya kutokea ugomvi kati yake na mkewe Mugabe, Grace Mugabe, na kusababisha kufutwa kazi na kukimbilia nchini Afrika Kusini.
Makamu huyo wa zamani wa rais ambaye alirejea kutoka uhamishoni siku ya Jumatano ataapishwa leo katika Uwanja wa Michezo wa Harare.
Kufutwa kwake kazi mwezi huu kulipelekea chama tawala cha Zanu-PF na jeshi kuingilia kati na kumlazimisha Mugabe ang'atuke .
Upinzani unamtaka Bwana Mnangagwa, ambae amekuwa mmoja wa watawala kumaliza "utamaduni wa ufisadi".
Taarifa ya kuondoka madarakani kwa Mugabe mwenye umri wa miaka 93 hapo siku ya Jumanne iliibua sherehe kubwa kote nchini Zimbabwe. Taarifa hiyo ilitolewa kwa njia ya barua bungeni na kikao cha kumpigia kura ya kutokuwa na imani nae kikakatizwa.
Katika barua hiyo Bwana Mugabe alisema anajiuzulu ili kuruhusu mchakato rahisi na wa amani wa ukabidhianaji mamlaka na kwamba uamuzi wake ulikuwa wa hiari.
Hayo yanajiri huku kukiwa na taarifa kwamba, Robert Mugabe amepewa kinga ya kutoshtakiwa sambamba na kudhaminiwa usalama wake ndani ya ardhi ya nchi hiyo. Duru za karibu na mazungumzo yaliyopelekea Mugabe kukubali kuachia madaraka zimefichua kuwa, Mugabe mwenye umri wa miaka 93 aliomba kuendelea kuishi Zimbabwe na kupewa usalama.