Waziri wa fedha wa Zimbabwe afikishwa mahakamani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36791-waziri_wa_fedha_wa_zimbabwe_afikishwa_mahakamani
Aliyekuwa waziri wa fedha wa Zimbabwe, Ignatius Chombo ambaye alikuwa amekamatwa na jeshi baada ya kuchukua mamlaka, leo amefikishwa mahakamani akikabiliwa na tuhuma za ufisadi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 25, 2017 12:48 UTC
  • Waziri wa fedha wa Zimbabwe afikishwa mahakamani

Aliyekuwa waziri wa fedha wa Zimbabwe, Ignatius Chombo ambaye alikuwa amekamatwa na jeshi baada ya kuchukua mamlaka, leo amefikishwa mahakamani akikabiliwa na tuhuma za ufisadi.

Kwa mujibu wa wakili wake, waziri huyo wa zamani wa fedha wa Zimbabwe anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi na utumiaji mbaya wa madaraka wakati alipokuwa waziri wa serikali za mitaa. 

Ignatius Chombo ni miongoni mwa maafisa wakuu wa serikali ya Zimbabwe waliokamatwa baada ya Robert Mugabe kuzuiliwa nyumbani kwake mnamo tarehe 14 Novemba.

Wakati huo huo, Mahakama Kuu  ya Zimbabwe imetangaza kuwa, hatua iliyochukuliwa na jeshi la nchi hiyo iliyopelekea kuondoka madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Robert Mugabe ilikuwa ya halali.

Taarifa ya mahakama hiyo imeeleza kuwa, hatua ya jeshi ya kuzuia kujilimbikizia mamlaka kwa wale waliokuwa karibu na Robert Mugabe ambako ni kinyume na katiba, ilikuwa ya mahala pake.

 Emmerson Mnangagwa, Rais wa Zimbabwe

Hayo yanajiri katika hali ambayo, jana Emmerson Mnangagwa, Makamu wa Rais wa Zimbabwe aliyefutwa kazi na Robert Mugabe wiki chache zilizopita aliapishwa kuwa rais mpya wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika na kuahidi kulijenga upya taifa hilo linalokabiliwa na mtikisiko mkubwa wa kiuchumi.

Jumanne iliyopita, Mugabe ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa miaka 37 alisalimu amri na kukubali kujiuzulu, kufuatia mashinikizo ya kila upande ya kumtaka aachie madaraka.

Emmerson Mnangagwa ataiongoza Zimbabwe hadi Septemba mwaka ujao 2018, wakati uchaguzi wa Rais utakapofanyika.