Azma ya Ulaya na Afrika ya kukabiliana na mgogoro wa wahajiri
Viongozi wa Ulaya na Afrika wametoa taarifa ya pamoja katika Mkutano wa Tano wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya huko Ivory Coast kuhusu mgogoro wa wahajiri barani Afrika na kusistiza udharura wa kupatiwa suluhisho la msingi suala hilo ikiwa ni pamoja na kupatikana ufumbuzi wa kisiasa wa mgogoro uliopo hivi sasa huko Libya.
Viongozi wa mabara hayo mawili wamesisitiza kupitia taarifa ya kisiasa waliyoitoa mwishoni mwa mkutano huo hapo jana mjini Abidjan azma yao ya kuwekeza katika nguvu ya vijana kwa ajili ya kuwa na mustakbali endelevu na katika uwanja huo, viongozi hao wametangaza vipaumbele vinne vya kistratejia vinavyojumuisha masuala ya kuwekeza kwa ajili ya marekebisho ya kimfumo na endelevu barani Afrika, kuwekeza kwa watu kupitia elimu, sayansi, teknolojia na kukuza vipawa, kuimarisha amani, usalama, utawala bora na hatimaye kusimamia suala la wahajiri.
Viongozi wa Kiafrika na Ulaya wameashiria pia vitendo visivyo vya kibinadamu vinavyofanywa na makundi ya wahalifu dhidi ya wahajiri na wakimbizi wa Kiafrika na kusisitiza udharura wa kupatikana suluhisho la kudumu la suala la wahajiri wa Kiafrika na kutatuliwa kwa njia ya kisiasa mgogoro wa Libya.
Afrika hivi sasa inakabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi, umaskini, ukosefu wa ajira, matatizo ya kiusalama, harakati za makundi ya kigaidi, vita na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, matatizo ambayo aghlabu yanasababishwa na siasa na uingiliaji wa nchi kigeni katika masuala ya bara la Afrika. Kwa miaka kadhaa sasa nchi za Magharibi zimejichimbia kwa njia ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja katika baadhi ya nchi za Afrika kwa visingizio mbalimbali kama kutetea haki za binadamu, kusaidia kurejesha amani na utulivu na kuendesha vita dhidi ya ugaidi. Miongoni mwa sasia zinazotumiwa na nchi za Magharibi na waitifaki wao barani Afrika ni kuwalinda na kuwahami baadhi ya viongozi wa nchi za Kiafrika ili waendelee kubakia madarakani, kuyauzia silaha na kuyaunga mkono kwa siri baadhi ya makundi ya kigaidi na kupora maliasili na utajiri ya madini ya nchi hizo.
Katika upande mwingine, kukosekana amani na utulivu wa kisiasa huko Libya na kutokowepo udhibiti mzuri wa maeneo ya mipaka ya nchi hiyo ni suala jingine lililowafanya wahajiri wengi wa Kiafrika kuchagua njia ya Bahari ya Mediterania na ile ya kuanzia katika pwani ya Libya kwa ajili ya kuelekea Ulaya. Pamoja na kuwa kabla ya hapa pia ripoti mbalimbali ziilifichua maafa ya kughariki wahajiri wa Kiafrika katika Bahari ya Mediterania na harakati za magenge ya magendo ya binadamu, lakini katika wiki kadhaa za hivi karibuni suala la kuuzwa wahajiri hao kama watumwa limewakasirisha sana viongozi wengi na taasisi mbalimbali za kutetea haki za binadamu duniani. Tatizo la wahajiri wa Kiafrika kuuzwa kama watumwa huko Libya limeshuhudiwa katika hali ambayo nchi za Magharibi na waitifaki wao ndio wamekuwa na nafasi na mchango mkubwa katika vita vinavyoendelea sasa nchini humo.
Kuhusu suala la wahajiri pia, siasa dhidi ya wahajiri zinazotekelezwa na nchi za Magharib hususan katika miaka kadhaa ya karibuni zimekuwa chanzo cha hali mbaya inayowakumba wahajiri wa Kiafrika.
Zaid Raad al Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa anasema kuhusu suala hilo kuwa: Chanzo kikuu cha mgogoro wa sasa na kushindwa kuwalinda wahajiri wa Kiafrika ni siasa za Umoja wa Ulaya dhidi ya raia hao.
Katika mazingira hayo, nchi za Magharibi, kwa mara nyingine tena, zimeshiriki kikao hicho kwa kaulimbiu ya kutoa misaada ya kibinadamu na kustawisha nchi za Kiafrka. Hata hivyo tunapotupia jicho ahadi zilizotolewa huko nyuma na nchi hizo tunaona kuwa Wamagharibi wanafuatilia malengo yao maalumu kama vile kudhibiti wahajiri wa Kiafrika na maliasili na utajiri wa bara hilo. Kwa msingi huo, baadhi ya viongozi wa Kiafrika wamelitaja chimbuko la matatizo ya bara hilo kuwa ni sera na siasa za madola ya kigeni na kusisitiza kuwa nchi za bara hilo zinapasa kufanya juhudi za kuyapatia ufumbuzi wa matatizo ya ndani na kuzidisha ushirikiano wa kieneo miongoni mwazo.