Mawaziri wawili wafutwa kazi siku mbili tu tangu wateuliwe nchini Zimbabwe
-
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe jana aliwafuta kazi mawaziri wake wawili zikiwa zimepita siku mbili tu tangu awateuwe siku ya Alkhamisi.
Serikali mpya ya Zimbabwe imesema kuwa, mawaziri hao wamefutwa kazi kama sehemu ya kuheshimu katibu ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, Mnangagwa amemfuta kazi Waziri wa Elimu, Lazaraus Dokora na nafasi yake kuchukuliwa na Paul Mavima; kama ambavyo pia amempiga kalamu Waziri wa Kazi, Clever Nyathi na nafasi yake kuchukkuliwa na Petronella Kagonye ambaye ni mbunge wa chama tawala cha Zanu-PF.
Mnangagwa aliapishwa kuwa rais mpya wa Zimbabwe tarehe 24 Novemba, yaani siku tatu baada ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Robert Mugabe kulazimishwa kujiuzulu.
Kujiuzulu Mugabe kulileta matumaini kwa wananchi wa Zimbabwe, hata hivyo taarifa zinasema kuwa wananchi hao hawakuridhishwa na uteuzi wa mawaziri uliofanywa na rais mpya kwani mawaziri wote wametoka katika chama tawala na ni sura zile zile za kipindi cha urais wa Robert Mugabe.
Si hayo tu, lakini pia Mnangagwa amewapa nafasi muhimu za uwaziri wa wizara nyeti majenerali wa kijeshi ambao walikuwa na nafasi kubwa katika kumlazimisha Mugabe ajiuzulu.