Mabadiliko ya kisiasa Zimbabwe baada ya Mugabe na mustakabali unaoikabili nchi hiyo
Baada ya kupita wiki chache tangu kuingia madarakani rais mpya wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa na kutangaza baraza lake jipya la mawaziri, malalamiko dhidi ya uteuzi aliofanya yamemfanya alazimike kuwabadilisha mawaziri wake wawili baada ya kupita siku mbili tu tangu alipowateua.
Lazaraus Dokora, ambaye aliteuliwa kuwa waziri wa elimu, ameondolewa na nafasi yake imechukuliwa na Paul Mavima. Naye Clever Nyathi, ambaye alitangazwa waziri mpya wa Kazi, amewekwa pembeni na nafasi yake imejazwa na Petronella Kagonye. Taarifa iliyotolewa na serikali ya Harare imeeleza kuwa kufanyika mabadiliko hayo lilikuwa jambo la lazima ili kuhakikisha hali hiyo inaendana na katiba, mazingira yanayohusiana na idadi ya watu na mahitaji mengine maalumu ya nchi.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, wataalamu wa siasa wanaitakidi kuwa rais wa Zimbabwe amechukua hatua hiyo kutokana na hasira za wananchi dhidi ya uteuzi aliofanya katika serikali mpya aliyounda nchini humo. Rais Mnangagwa amekosolewa vikali kwa kuwateua tena viongozi waliohudumu kwenye serikali iliyopita ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Robert Mugabe aliyeondoka madarakani baada ya kulazimika kujiuzulu na vilevile kuwapatia nyadhifa nyingi za uongozi maafisa wa jeshi la nchi hiyo. Kwa upande mwengine rais mpya wa Zimbabwe hakutoa nafasi zozote muhimu za uongozi kwa wapinzani bali nyadhifa zote za uwaziri amewapa maveterani wa vita vya uhuru wa nchi hiyo. Nelson Chamisha, afisa wa chama cha upinzani cha MDC amelizungumzia suala hilo kwa kusema: "sisi tumevunjwa moyo na jambo hili, kwa sababu Emmerson Mnangagwa hakukidhi matarajio ya Wazimbabwe. Tulikuwa na matumaini ya kushuhudia baraza la mawaziri litakalokidhi matarajio ya wananchi. Tulitarajia kuona sura mpya."
Rais Mnangagwa amefanya uteuzi huo uliolalamikiwa na wananchi ilhali wakati wa sherehe za kuapishwa kuwa rais mpya wa Zimbabwe aliahidi kuleta demokrasia na kufanya mabadiliko ya msingi nchini humo.
Hata hivyo, kabla Mnangagwa hajaanza kazi rasmi kama rais mpya wa Zimbabwe, wachambuzi wengi walikuwa wameshatabiri kwamba kuja kwake madarakani hakutaleta mabadiliko makubwa katika mazingira na hali ya ndani ya nchi hiyo, kwa sababu yeye ni miongoni mwa watu wa karibu na Mugabe na wanaofanana naye kiuongozi kiasi kwamba msemaji wa chama cha MDC amewaelezea Mugabe na Mnangagwa kuwa ni sawa na pande mbili za sarafu moja. Pamoja na hayo kuna watu wengi pia ambao walikuwa na matumaini ya kutokea mabadiliko nchini Zimbabwe katika muelekeo wa kuboreshwa mazingira ya kisiasa na hali ya uchumi wa nchi.
Hivi sasa hali mbaya ya uchumi wa Zimbabwe imesababisha kuongezeka kiwango cha watu wasio na ajira na kuchochea malalamiko ya kisiasa na kijamii. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, kiwango cha umasikini nchini humo kimefikia asilimia 72 na cha ukosefu wa ujira kimefikia asilimia 82. Alipohutubia baada ya sherehe za kuapishwa, rais Mnangagwa aliahidi kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira na kuongeza kasi ya msukumo wa gurudumu la uchumi. Aidha aliahidi kuwa ataelekeza juhudi zake katika kuvutia tena wawekezaji wa kigeni. Kuhusiana na suala hilo, Gift Maguano, mtaalamu wa masuala ya uchumi anasema: serikali mpya inatakiwa irekebishe au kubadilisha kikamilifu baadhi ya sera za Robert Mugabe ikiwemo ya kutegemea mitaji na uwekezaji wa ndani tu, kwa sababu hakuna suhula na uwezekano wa kuwekezwa vitega uchumi vya ndani ya nchi.
Kwa ujumla inapasa tuseme kuwa hivi sasa kipindi kipya cha kisiasa kimeanza nchini Zimbabwe, ambapo kama utendaji wa Mnangagwa utakuwa chanya ataweza kuboresha hali za maisha ya watu na kuwafanya wawe na imani na chama tawala cha Zanu-PF; vinginevyo wapinzani watapata fursa tena ya kuwahamasisha kuingia barabarani wananchi wasioridhishwa na utendaji wa serikali ya chama hicho.../