Puntland yatangaza hali ya hatari kutokana na ukame
(last modified Wed, 06 Dec 2017 07:54:04 GMT )
Dec 06, 2017 07:54 UTC
  • Puntland yatangaza hali ya hatari kutokana na ukame

Eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland nchini Somalia limetangaza hali ya hatari kutokana na kushtadi ukame, huku likiiomba jamii ya kimataifa msaada wa chakula na maji.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Puntland hapo jana imesema asilimia 70 ya watu wa eneo hilo wanasumbuliwa na ukame na kwamba hakuna dalili zozote za kushuhudiwa mvua katika kipindi cha miezi mitano ijayo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, familia 34,000 katika eneo hilo zinakabiliwa na baa la njaa lililosababishwa na janga hilo la kimaumbile.

Baada ya watu 110 kufariki dunia kutokana na njaa nchini Somalia mwezi Machi mwaka huu, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea maafa makubwa katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kama yale ya mwaka 2011 ambayo yalisababisha vifo vya malaki ya watu.

Ramani inayoonyesha eneo la Puntland la Somalia

Ripoti zinaonyesha kuwa, zaidi ya nusu ya wakazi wa eneo jingine lililojitangazia mamlaka ya kujitawala la Somaliland wanakabiliwa na hali mbaya ya ukame na njaa.

Takwimu na ripoti za mashirika ya kimataifa zinaonesha kuwa, zaidi ya watu milioni 40 katika nchi nyingi za Afrika wameathiriwa na njaa na ukame uliosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa ya El-Nino.