Mwanasheria Mkuu wa Kenya amuonya Odinga dhidi ya kujiapisha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37303-mwanasheria_mkuu_wa_kenya_amuonya_odinga_dhidi_ya_kujiapisha
Mwanasheria Mkuu wa Kenya ametahadharisha kuhusu mpango wowote wa kumuapisha kinara wa upinzani nchini humo Raila Odinga kama 'rais wa watu' wiki ijayo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 07, 2017 15:00 UTC
  • Mwanasheria Mkuu wa Kenya amuonya Odinga dhidi ya kujiapisha

Mwanasheria Mkuu wa Kenya ametahadharisha kuhusu mpango wowote wa kumuapisha kinara wa upinzani nchini humo Raila Odinga kama 'rais wa watu' wiki ijayo.

Profesa Githu Muigai amesema kumuapisha Odinga ni kinyume cha sheria na kitendo ambacho kitampelekea mwanasiasa huyo mkongwe akabaliwe na shitaka la uhaini.

Profesa Muigai ambaye ni mshauri mkuu wa serikali katika masuala ya sheria amesema kumuapisha Odinga ni kinyume na katiba kwa kuwa nchi hiyo tayari ina rais halali.

Kadhalika amewaonya viongozi na wafuasi wa upinzani wenye azma ya kushiriki hafla za kuapishwa Odinga, akisisitiza kuwa watakabiliwa na mkono wa sheria.

Raila Odinga

Novemba 28, masaa machache baada ya Rais Kenyatta kula kiapo kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 ambao ulisusiwa na Odinga, kinara huyo wa NASA alisema ataapishwa kuwa rais 'halali' wa Kenya Disemba 12, wakati nchi hiyo itakuwa inaadhimisha Siku ya Jamhuri.

Uchaguzi huo wa marudio ulifanyika baada ya Mahakama ya Juu kubatilisha uchaguzi wa Agosti 8, ikisema kuwa uligubikwa na kasoro nyingi na kuwa haukuzingatia miongozo ya sheria na katiba. 

Kenyatta akiapishwa kuhudumu muhula wa pili na wa mwisho

Indhari ya Mwanasheria Mkuu wa Kenya imekuja masaa machache baada ya Raila Odinga kuikosoa vikali serikali ya Marekani ambayo imemtaka ajiepushe na azma hiyo ya kuapishwa, akisisitiza kuwa Washington haina itibari ya kuzungumza chochote kuhusu siasa za Kenya kwa kuwa ilifumbia macho mauaji ya makumi ya waandamanaji katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki tangu mwezi Agosti mwaka huu.