Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusu ukame na njaa Sudan Kusini
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kibinadamu ametahadharisha kuhusiana na kuzidi kuwa mbaya hali ya chakula kwa zaidi ya watu milioni moja huko Sudan Kusini.
Mark Lowcock amesema hayo katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kutangaza kuwa, zaidi ya watu milioni moja na laki mbili huko Sudan Kusini wanajongewa na ukame na baa la njaa na kwamba, idadi ya watu hao imeongezeka maradufu ikilinganishwa na mwaka jana katika kipindi hiki hiki cha mwaka.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kuna maeneo kadhaa ya Sudan Kusini ambayo yumkini katika miezi michache ijayo yakakumbwa na ukame na uhaba mkubwa wa chakula.
Kwa mujibu wa Idara ya Taifa ya Takwimu nchini Sudan Kusini, asilimia 56 ya raia wa nchi hiyo changa barani Afrika, sawa na watu milioni 6 wanakabiliwa na baa la njaa.
Hali hii ya njaa pamoja na machafuko yamesababisha maelfu ya raia wa Sudan Kusini waendelee kumiminika katika nchi jirani za Sudan na Uganda wakitafuta chakula na mahala salama pa kuishi.
Sudan Kusini ilitumbukia kwenye mgogoro mkubwa tangu Rais Salva Kiir alipomtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar kuwa alipanga njama za kumpindua mwezi Disemba 2013. Makumi ya maelfu ya watu wameshauawa na mamilioni ya wengine kupoteza makazi yao kutokana na machafuko yaliyoikumba nchini hiyo changa zaidi duniani.