Sisisitizo la Ufaransa na Misri la kuimarisha uhusiano wao wa kijeshi
Paris na Cairo zimesisitizia azma yao ya kuimarisha ushirikiano baina yao katika nyuga tofauti za kijeshi na kiusalama.
Rais Abdul Fattah el Sisi wa Misri na Bi Florence Parly, waziri wa ulinzi wa Ufaransa, wamekutana mjini Cairo na kuzungumzia njia za kuimarisha ushirikiano wa pande mbili hususan katika masuala ya kijeshi na kiusalama.
Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, viongozi wa Misri na Ufaransa wamefanya safari nyingi za kutembeleana kama sehemu ya kuimarisha uhusiano wa nchi zao. Vita dhidi ya ugaidi, kuongezwa biashara ya vifaa na zana za kijeshi na kustawishwa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara ndiyo malengo makuu ya safari za mara kwa mara za pande mbili za viongozi wa nchi hizo. Katika ziara ya hivi sasa ya waziri wa ulinzi wa Ufaransa nchini Misri, ajenda kuu ya safari hiyo ni kuandaliwa mazingira ya kukuza ushirikiano wa kijeshi na kiusalama hususan kununua Misri silaha kutoka Ufaransa.
Michel Cabirol, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Lengo la ziara ya waziri wa ulinzi wa Ufaransa huko Cairo ni kuandaa mazingira ya ziara ya Macron nchini Misri na vile vile kutiwa saini mikataba ya kijeshi baina ya nchi mbili.
Tangu mwaka 2015, Misri imeongeza kiwango cha manunuzi ya silaha kutoka nchini Ufaransa. Katika kipindi hicho, Cairo imenunua ndege 24 za kivita aina ya Rafale, manuari moja na meli mbili za kivita pamoja na makombora mengi, zana za kijeshi ambazo zinakadiriwa kuwa na thamani ya takriban euro bilioni 5 na milioni 200 kutoka nchini Ufaransa.
Hivi sasa viongozi wa Misri wako katika harakati za kutiliana saini mikataba mipya ya silaha na kuongeza kiwango cha ushirikiano wao wa kijeshi na Ufaransa. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kuongezeka mashambulizi ya kigaidi nchini Misri kumeandaa mazingira mazuri na kisingizio cha kutosha cha kununuliwa silaha nyingi zaidi za kivita huko Misri.
Mokhtar Awadh, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Lengo kuu la magenge ya kigaidi yanayofanya mashambulizi yao kwa mpangilio maalumu huko Misri, ni kuzusha hali ya wasiwasi na ukosefu wa utulivu katika nchi hiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu kwenye eneo hili na matunda yake ni kulazimika Misri kununua silaha nyingi kutoka kwa nchi za Magharibi.
Katika upande mwingine, viongozi wa Cairo wana nia ya kuimarisha nafasi yao kijeshi katika siasa zao za kiistratijia kwenye ulimwengu wa Kiarabu na katika eneo la kaskazini mwa Afrika.
Kustawishwa uhusiano wa Misri na Ufaransa na hususan katika upande wa ushirikiano wa kiusalama na kupambana na ugaidi, kuna umuhimu mwingine mkubwa usiokuwa huo tulioutaja nao ni kwamba, viongozi wa Ufaransa wanajaribu kutumia kisingizio cha kupambana na ugaidi katika eneo hili hususan Misri ili kupunguza nguvu za kupenya magaidi barani Ulaya.
Hata hivyo juhudi za kuimarisha uhusiano baina ya Misri na Ufaransa zinafanyika katika hali ambayo, hivi sasa kivuli kimetanda katika uhusiano wa nchi hizo mbili hususan linapofika suala la haki za binadamu. Ripoti nyingi za kimataifa zinawalaumu viongozi wa Misri kuwa wanakanyaga haki za binadamu na kuwapokonya Wamisri uhuru wa kisiasa. Ni kwa sababu hiyo ndio maana taasisi na mashirika mengi ya kimataifa ya haki za binadamu yakawa yanailaumu Ufaransa kwa kuimarisha uhusiano wake na Misri yakisema kuwa, si tu viongozi wa Paris wanafumbia macho uvunjaji wa haki za binadamu unaofanyika nchini Misri, bali hata wanazidi kuwaimarisha kwa nguvu za kijeshi na kiusalama viongozi wa nchi hiyo kwa madai ya kupambana na ugaidi. Hata hivyo ukosoaji huo hauonekani kupunguza kasi ya kuimarisha uhusiano wa nchi mbili hizo hususan katika masuala ya kijeshi na kiusalama. Ziara ya hivi sasa ya waziri wa ulinzi wa Ufaransa huko Misri ni mfano wa wazi wa jambo hilo.