UN yafikia uamuzi wa kuwaondoa wahajiri nchini Libya
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema kuwa umoja huo umefikia uamuzi wa kuwaondoa wahajiri nchini Libya na kuwapeleka katika nchi ya tatu.
Mtandao wa gazeti la Le Monde la nchini Ufaransa umeinukuu ofisi ya UNHCR ikisema kuwa, kwa kuzingatia hali mbaya ya wahajiri nchini Libya, Umoja wa Mataifa umeamua kuwahamishia barani Ulaya baadhi ya wahajiri hao na inatabiriwa kuwa ifikapo mwaka 2018 wahajiri baina ya elfu tano hadi 10 watakuwa wameshahamishiwa barani humo.
Umoja wa Mataifa umezitaka nchi za Ulaya kutekeleza majukumu yao kuhusiana na wahajiri hao baada ya kuenea mkanda wa video ya matukio ya kweli uliorushwa hewani na televisheni ya CNN ukionesha namna wahajiri wa Kiafrika wanavyopigwa mnada sokoni na kuuzwa kama watumwa huko Libya.
Kwa upande wake, Umoja wa Afrika AU nao ulitoa tamko mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba na kuahidi kuwa utawarejesha makwao wahajiri 20 elfu waliokwama nchini Libya katika kipindi cha wiki sita tangu lilipotolewa tamko hilo.
Baadhi ya vyombo vya habari vilitangaza kuwa, wahajiri wa Kiafrika wanauzwa kwa dola 400 nchini Libya kama watumwa na wanunuzi wakuu wa wahajiri nao ni wamiliki wa mashamba.
Mgogoro huo mkubwa wa wakimbizi ambao haujawahi kutokea mfano wake duniani umetokana na siasa za kivamizi za nchi za Magharibi na vibaraka wao hasa katika nchi za Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika.