Mnangagwa amteua aliyekuwa mkuu wa jeshi Zimbabwe kuwa naibu wake
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amemteua Kamanda wa Vikosi vya Ulinzi aliyetangaza kujiuzulu wadhifa huo siku chache zilizopita, Jenerali Constantino Chiwenga kuwa naibu wake ndani ya chama tawala Zanu-PF.
Wadadisi wa mambo wanasema Jenerali Chiwenga amepewa wadhifa huo kama bakhshishi ya kuongoza mapinduzi baridi ya kijeshi yaliyomlazimisha Robert Mugabe kutangaza kujiuzulu na kung'atuka madarakani.
Aidha Mnangagwa amemteua mwanasiasa mkongwe nchini humo, Kembo Mohadi kuwa naibu wake wa pili ndani ya chama hicho tawala.
Msemaji wa Rais wa Zimbabwe, George Charamba amesema uteuzi wa wawili hao kuwa makamu wa rais wa nchi unaweza kufanywa tu na Katibu Mkuu wa serikali na baraza la mawaziri, Misheck Sibanda ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi.
Mnangagwa aliapishwa kuwa rais mpya wa Zimbabwe tarehe 24 Novemba, siku tatu baada ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Robert Mugabe kulazimishwa kujiuzulu.
Kujiuzulu Mugabe kumeleta matumaini kwa wananchi wa Zimbabwe, hata hivyo taarifa zinasema kuwa wananchi hao hawajaridhishwa na uteuzi wa mawaziri uliofanywa na Mnangagwa hivi karibuni, kwani mawaziri wote wametoka katika chama tawala na ni sura zile zile za kipindi cha urais wa Mugabe.